UKIINGIA KWENYE NDOA NA MWENYE SIFA HIZI HUWEZI KUJUTA
Mara nyingi tunapofikiria namna ya kumpata mwenza sahihi, huwa tunaangalia ishu ya kumpata yule mwenye mapenzi ya dhati lakini kumjua anayekupenda kwa dhati, anayeweza kukupatia kile ulichokitarajia ni vigumu sana.
Ndiyo maana hapa chini nimekupa vigezo saba vya mtu ambaye anakupenda kwa dhati na anafaa kuwa mwenza wako endapo mtakuwa tayari mmeshaanzisha uhusiano wa kawaida.
MGUSO WA HISIA
Hakika mapenzi ni mguso wa hisia, kwa maana hiyo kigezo kikuu cha kuzingatia kwa mtu anayestahili kuwa mwenzi wako wa ndoa ni vile ambavyo hisia zake umeziteka. Hali kadhalika na wewe mwenyewe ulivyotekwa naye.
Amani na furaha vikitawala kati yenu unajiona upo huru kwa kila kitu na mnapokuwa hamuelewani kila kitu kwenye akili yako unaona hakiendi. Vivyo hivyo na yeye kwamba amani ipo pale mnaelewana na inatoweka mnapokosana. Huyo ni wazi mnaendana.
KUTOSHEKA
Ukiwa naye unajisikiaje? Umetosheka eeh? Akiwa mbali inakuaje, unahisi kuna upungufu mkubwa? Vipi na yeye anajiona hivyohivyo? Kama jibu ni ndiyo maana yake mnaendana kwa sababu ukamili wako unamtegemea yeye, hali kadhalika na yeye.
Anakata kiu yako yote? Na upande wake inakuaje? Ikiwa ni hivyo, basi anatosha kuwa mwenzi wako wa maisha.
MALENGO
Kila mtu anapoingia kwenye uhusiano wa kimapenzi, lengo lake huwa ni kudumu. Achana na hulka za viruka njia. Pointi hii inakujenga kujua matarajio ya mwenzako kuhusu wewe. Anakuhitaji kwa maisha yake yote au yupo na wewe kwa sababu hana pa kwenda?
Wengi wapo kwenye majuto kwa sababu waliingia kwenye ndoa na watu ambao hawakuwa na nia ya dhati nao, bali walijichanganya baada ya kukosa uelekeo.
ISHU YA MAWASILIANO
Anapenda kuwasiliana na wewe, ukimtumia SMS anaijibu ‘fasta’. Hatengenezi sababu ya kutowasiliana na wewe, daima anaona njia pekee ya kuwaweka karibu hata kama mpo mbali ni kuwasiliana. Nawe unampigia simu kwa wakati, unasikia raha kupokea ujumbe wake naye anaona fahari kupigiwa simu na wewe.
Kama hali hiyo ipo, basi upendo wa kweli upo na hiyo inatosha kuthibitisha kwamba mnaendana. Ukituma SMS naye akachelewa kujibu ni wazi haoni umuhimu wako.
NI WA SHIDA NA RAHA
Hapa ni hisia tu, ikiwa mnapendana kwa dhati basi akiumia nawe yatakuwa ni maumivu yako. Ikiwa hauna raha halafu yeye ni mwenye furaha basi huyo anakupenda kinafiki. Hatofautiani na yule anayebembeleza ndoa ili kuondoa mkosi. Kuwa makini, hakikisha unakuwa na mtu ambaye ni wa shida na raha.
ANAJUTA NA KUOMBA MSAMAHA
Mpenzi bora ni yule anayejutia kosa pale anapokukosea, pia anaomba msamaha. Hapa ieleweke kuwa kuomba msamaha peke yake haitoshi, isipokuwa anapaswa kuonesha wazi kwamba ametambua makosa yake na amejuta.
Kimsingi mtu mwenye sifa hiyo huwa hasumbui mnapokuwa ndani. Epuka mtu mbishi, anakosea na hatambui kosa lake na badala yake anajenga hoja.
HAYUKO TAYARI KUKUKOSA
Mnagombana anaumia lakini bado yupo na wewe. Anakuonesha waziwazi kuwa hayupo tayari kuachana nawe. Yupo radhi kutumia muda mwingi kutafuta suluhu ili muendelee kuwa pamoja. Hiyo inaonesha kuwa anakupenda kwa moyo mmoja.
Mtu mwenye moyo mgumu, mnagombana wala hashtuki na hatengenezi mazingira ya kurudiana, maana yake hana hisia za kweli, na anavyokuchukulia ni kwamba hata mkiachana yeye anaona sawa.
JIANGALIE NA WEWE!
Umeangalia yote hayo, sasa jiangalie na wewe mwenyewe. Moyo wako unakusukuma kuwa na yeye? Hilo ndilo swali la msingi kwa sababu mapenzi hayataki majaribio, ukiingia ndiyo imetoka. Yanini kujipa kumbukumbu mbaya baadaye?
Maisha bora au mabaya ya baadaye yanatokana na uamuzi wa leo, mwenzi sahihi wa maisha ni mbolea ya furaha ya kudumu baadaye. Kwa hiyo kabla hujaingia kwenye uhusiano wa ndoa ni vema kujiuliza mara mbilimbili.
No comments