Breaking News

Fahamu Maana ya Vifupisho vya Maneno Vinavyotumika Sana Kwenye Mitandao ya Kijamii

Ni ukweli usiopingika kwamba maendeleo ya sayansi na teknolojia, yamefanya matumizi ya intaneti kuongezeka sana. Matumizi ya intaneti nayo yamekuja na mambo mapya, katika ulimwengu wa sasa, mawasiliano kupitia mitandao ya kijamii, kama Facebook, Instagram, Whats App na kwingineko ni kitu cha kawaida kabisa.
Sasa mambo mapya yanakuja na changamoto mbalimbali! Miongoni mwa changamoto kubwa inayowasumbua wengi, ni lugha zinazotumika kimataifa kwenye mitandao ya kijamii. Sote tunafahamu kwamba lugha kuu ya kimataifa kwa huku kwetu ni Kiingereza.
Unaweza kuwa unakijua Kiingereza lakini kwa sababu ya ugeni wa maneno fulani, ukajikuta ukiachwa kwenye mataa.
Hebu chukulia mfano, umepost picha yako Facebook au Instagram, halafu anakuja mtu ana-comment kwa kuandika LMFAOO! Au SMH!
Unajua kiingereza ndiyo, lakini unaweza kuyaelewa maneno hayo? Hiyo ndiyo sababu iliyonifanya leo nikaja na mada hii, naamini itakuwa muhimu sana kwako.
VIFUPISHO NA MAANA ZAKE
-OMG- Ooh! My God (Ooh! Mungu Wangu!)
Maneno haya hutumika kuonesha jinsi ulivyopatwa na mshtuko, uwe wa jambo la furaha au jambo la kushtua.
LMAO- Laugh My A** Off (Nimecheka mpaka basi!)
Neno hili siyo rasmi na lina lugha ya ukakasi ndani yake kutokana na neno moja lililopo ndani yake lakini kwa kifupi, huwa linamaanisha kwamba ‘nimecheka mpaka basi’. Hii hutumika pale unapochangia kitu kwenye mitandao ya kijamii,ukionesha kwamba umefurahishwa mno na alichokisema au alichopost mtu aliyekutangulia.
LMFAO- Laugh My F**king A** Off (Nimecheka sana mpaka basi)
Hii pia ina maana ileile kama LMAO ila hapa ni kuongeza msisitizo lakini pia kuna neno jingine lenye ukakasi zaidi limetumika. Wenzetu Wamarekani, hasa katika lugha za mitaani, mtu anapofurahi sana hutumia matusi kuwasilisha furaha yake na hicho ndicho kinachoonekana kwenye LMAO na LMFAO.
Haina maana kwamba kwa sababu vifupisho hivyo vina maneno ya ukakasi basi mtu akikwambia anakutukana, hapana, anaonesha ni jinsi gani alivyofurahi.
ROFL- Rolling On the Floor Laughing (Nimegalagala kwa kicheko)
Hii pia ina maana zinazoshabihianana LMAO na LMFAO. Kuna ile hali ambayo mtu anaweza kucheka mpaka akakaa chini au kugalagala sakafuni! Basi hiki ndicho kinachomaanishwa kwenye ROFL! Unacheka mpaka unagalagala chini.
LOL- Laughing Out Loud- (Kucheka kwa sauti)
Wakati mwingine unaweza kuwa unaperuzi simu yako lakini ghafla ukakutana na kitu ambacho kitakufanya ucheke kwa sauti na kuwashtua watu walio karibu na wewe! Sasa hii ndiyo LOL, kucheka ghafla kwa sauti, hasa katika mazingira ambayo hata wewe hukutegemea kama utacheka.
SMH- Shake My Head (Kutingisha Kichwa)
Wakati mwingine, unaweza kukutana na kitu ambacho kitakufanya utikise kichwa chako, inaweza kuwa ni kitu cha kijinga sana, au kitu cha kufurahisha sana au kitu cha kukufanya umsikitie aliyefanya kitu hicho. Basi ukiona mtu ameposti na kuandika herufi hizo tatu tu, SMH tambua kwamba hicho ndicho alichokuwa amekimaanisha.
BFF- Best Friend Forever (Rafiki Bora wa Kudumu)
Unaweza kukuta mtu ameposti picha ya mtu fulani halafu akasindikiza na maneno BFF! Au kuna picha ya mtu akiwa na rafiki yake. Hii humaanisha kwamba hao wanaoonekana kwenye picha hiyo, au huyo aliyepostiwa ni rafiki bora na wa kudumu wa mhusika.
HASHTAGS (#)
Watumiaji wa mitandao ya kijamii, wana kitu kinachoitwa Hashtags (#) ambapo hapa mtumiaji yeyote anaweza kuandika chochote akitangulia kwa kuandika alama ya hash (#) kisha kile alichokiandika kwenye neno la kwanza, kitaungana na walichokiandika watu wengine wengi kuhusu mada hiyohiyo, kwa lugha ya Kitaalamu hapo unakuwa ume-join conversation na watu kutoka sehemu mbalimbali duniani wanaozungumzia kitu ulichokiandika.
Kwa mfano, ukiwa Twitter unaweza kuandika #Trump, utakachokiandika kitaonekana dunia nzima na wewe utaona wenzako walichokiandika kuhusu Trump. Vivyo hivyo ukiandika #Sudan, utaona mambo chungu nzima yaliyoandikwa kuhusu nchi ya Sudan.
Sasa katika Hashtags maarufu, zipo zile saba ambazo zimegawanywa kwa siku tofautitofauti, kuanzia Jumatatu mpaka Jumapili, hapa tutaziangalia chache ambazo ni maarufu zaidi.
TBT- Throw Back Thursday (Alhamisi ya ‘Zilipendwa’)
Wengi wamezoea tu kusema TBT lakini ukiwauliza maana yake, wataishia kukutazama usoni. TBT maana yake ni Throw Back Thursday ikimaanisha Alhamisi ya kukumbushia matukio ya siku zilizopita, inaweza kuwa mwaka jana, mwaka juzi, miaka kumi iliyopita na kadhalika. Sheria moja ya TBT lazima iwe ni siku ya Alhamisi.
MCM- Man Crush Monday (Mwanaume Anayenivutia Jumatatu)
Hii inawahusu zaidi wanawake. Jumatatu huwa ni siku yao ya kuonesha ni mwanaume gani anayemvutia zaidi, pengine kimapenzi, kimwonekano, kiundugu na kadhalika. Kwa hiyo kila Jumatatu, utakuta wanawake wapo bize Instagram, Twitter na kadhalika, kila mmoja akiposti picha ya mwanaume anayemkubali na kusindikiza na #MCM (Hashtag Man Crush Monday).
WCW- Woman Crush Wednesday (Mwanamke Anayenivutia Jumatano)
Hii ni kama MCM isipokuwa hii inawahusu zaidi wanaume na huwa ni siku ya Jumatano, ambapo wanaume utakuta wapo bize huko mitandaoni, kila mmoja akiposti picha ya mwanamke anayemvutia, awe ni mkewe, mpenzi wake, mama yake, binti yake na kadhalika huku akisindikiza na #WCW.
TGIF- Thank God Its Friday (Ahsante Mungu Ijumaa Imefika)
Hii inawahusu zaidi wale wapenda bata, ambao kwao kujirusha kuna maana zaidi kuliko kufanya kazi (natania!). Inapofika Ijumaa, watu wengi hawa wafanyakazi hufurahi sana kwa sababu wikiendi imefika, muda wa kupumzika na kufurahi mpaka Jumapili kabla ya Jumatatu kuingia tena kazini. Sasa inapofika Ijumaa kuanzia mida ya saa nne asubuhi, mitandao ya kijamii huanza ‘kuchafuka’ kwa picha za kufurahisha kuhusu watu wanavyofurahia wikiendi huku wakisindikiza na #TGIF.
Picha nyingi ambazo hupostiwa, huonesha vibonzo vya jinsi watu wanavyoyakimbia mafaili ofisini na kuelekea kwenye burudani, picha za pombe, burudani za hapa na pale na kadhalika.
Kimsingi hii huwa ni siku inayopendwa sana na wafanyakazi wa maofisini kwa sababu sasa ni kama wanafunguliwa kutoka kwenye kifungo cha siku za kazi.
EMOJI
Hivi ni vile vipichapicha vinavyotumika kwenye mitandao ya kijamii kuwasilisha ujumbe mkubwa kwa kapicha kamoja tu. Mtu anaweza kutumia ka-emoji ka mtu anayecheka akimaanisha amecheka kwa kilichopostiwa, emoji ya kulia akimaanisha amehuzunishwa sana na kilichopostiwa na kadhalika.
Emoji zipo nyingi na zinatumika zaidi kwenye mtandao wa WhatsApp na jambo ambalo kila mmoja anapaswa kulijua ni kwamba kila emoji huwa ina maana yake na hutumika sehemu mahsusi, zipo nyingine ambazo huwa zinatumiwa na wanaume tu na zipo nyingine ambazo hutumiwa na wanawake tu

No comments