NILAMBE TENA….3
“Nimekuelewa Lina. Lakini mbona zimebaki siku chache kwa wewe
kuondoka? Hiyo kazi nitaikamilisha vipi?”
nilimuuliza Lina wakati huo akipaki gari
pembeni ambapo sikuchelewa
kumbandika swali linguine kabla
hajanijibu ya awali. “Mbona unapaki kabla hatujafika? Au
umeona sehemu iliyobakia nitembee kwa
mguu?”
“Si kweli maswali yako na vilevile
nikikujibu nitakudanganya kwa wakati
huu. Cha muhimu yatazame macho yangu halafu utajua nini namaanisha na
kipi nakihitaji toka kwako.” Nikamtazama
kama alivyotaka. Macho yake malegevu
kama vile kipo alichokula kuyalegeza
zaidi. Lakini pamoja na kumuangalia
moyo wangu ulikuwa ukinienda mbio. Lina hakuwa na haraka kama mama
yake. Kudhihirisha usomi wake, akanihoji
swali lililonitia kigugumizi.
“Una mahusiano ya kimapenzi na mama
yangu?” niweke wazi nilishindwa kumjibu
swali lake. Niliogopa kumdanganya. Nikahamishia macho yangu chini.
Sikutaka kumtizama tena usoni.
“Namfahamu vyema mama yangu.
Kwahiyo usiogope kunijibu. Huenda jibu
lako kwangu likakuepusha na mengi.”
Hapo alinishtua kidogo. Litakalotokea basi! Nilijisemea kabla ya kumjibu.
Nasema hivyo kwasababu hadi wakati
huo hata kama ningekorofishana nao,
sikuwa na lolote la kupoteza kwao.
“Hapana. Ila leo nd’o ilikuwa tuweke
uhusiano. Wewe ndiye umevuruga.” Baada ya jibu langu, akapandisha vioo
vya pande zote kisha akaniomba namba
ya simu yangu. Nikampatia. Akaondoa
gari kwa kasi kufuatana na vile
nilivyomuelekeza. Akanifikisha nyumbani
na kuniaga. Nikaingia ndani kwangu na kujitupa kitandani kwasababu ya kuhisi
usingizi.
Kilichonishtua ni simu yangu kuita.
Wakati nikilala, niliisahau mfukoni.
Nikaingiza mkono mfukoni na kuitoa.
Namba ilikuwa ngeni lakini haikunishtua kwasababu kazini kwangu niliiandika juu
ya mlango kwaajili ya wateja wakinihitaji
nisipokuwepo kazini. Nikapokea na
kuiweka sikioni.
“Habari yako kijana” ilisikika sauti ya
mwanaume. Dah! Nilitamani nimvute kwenye simu muda uleule nimchape
vibao. Mwenziye nilitaraji ni Lina. Kumbe
sauti nzito kama injini ya meli. Loh!!
“Nzuri.” Nilimjibu lakini nikitamani akate
simu muda uleule.
“Nilikuja leo kazini kwako haukuwepo. Shida yangu si kubwa sana lakini inayo
malipo mazuri. Naamini wewe ni
mtaalamu wa kuziremba kucha za
wanawake. Nilitaka uzifanyie mambo
kucha za mke wangu maana tuna safari
siku mbili zijazo.” Aliongea cha maana. Si kazi jamani? Nani anayechukia kufanya
kazi ya fedha? Kama upo wa aina hiyo
basi hustaili katika nchi yetu na hata kwa
wenzetu. Tulikubaliana kesho yake
nikaifanye kazi yake kama alivyoihitaji.
Akakata simu nami nikateremka kitandani na kuandaa maji ya kwenda
kuoga.
Nilipomaliza kuoga na kubadili nguo,
nilitoka na kwenda kupata chochote
tumboni mwangu. Hayo ndiyo yalikuwa
maisha yangu ya kila siku. Chumbani kwangu sikuwa na kikombe wala sufuria.
Ndoo na beseni kwa ajili ya kufulia,
pamoja na jagi ili asubuhi niweze
kuswaki pasipo tabu. Sikuwa nikipika
wala sikutamani linizoee kabisaa neno
kupika. Maisha ya kula hotelini sikuyachoka kwasababu niliyachagua
mwenyewe. Kama umepanga kama mimi
usiniige katika hilo kwakuwa usiwaone
wacheza mpira ukadhani wote
wanafaidika nao. Pole!!
“Umelala? Ilikuwa ni meseji iliyoingia katika simu yangu baada ya kutoka kula
na kujilaza kitandani. Mwishoni mwa
meseji ile, alijitambulisha mtumaji ili
asinipe tabu ya kuuliza ni nani maana
namba ilikuwa ngeni. Siyo mdada
unadundadunda kitaani unajiita mjanja wa town vitu kama hivyo huvijui. Muda
wa kuandika sms ya kuulizwa wewe nani,
huenda angekutumia hata meseji ya
kukusifia. Alaa! Unamchosha mtu buana.
“Bado sijajikunyata Lina lakini nipo
kitandani.” Nilimjibu. “Poa.” Ehee! Nikashangaa mtu kanianza
yeye lakini kwa muonekano kama vile
alinikatishia juu kwa juu. Yupo sahihi.
Mwanamke pozi. Kama huna pozi basi
pole yako maana hata mnyama jike
lazima amsumbue dume weeee. Wakimbizane weee mpaka. Maksudi
ilikuwa ni kunipatia namba yake. Sasa
kamaliza acha mjomba nianze kutupa
tufe. Lakini najikakamua kwasababu
nilishaona yupo tayari. Hivyo mimi ni
kumalizia tu mpira ndani ya nyavu kwakuwa golikipa alishakata upepo
upande wa kushoto. Unajua kwanini
nakwambia kurusha tufe? Siyo zile
mambo za ooo nakupenda kama moyo
wangu. Unampenda kama moyo wako?
Acha uongo basi ndugu yangu maana moto ukizuka ndani hutasubiri atoke
ndipo ufuatie wewe. tena huenda
ukampiga hata kikumbo uanze kutoka
wewe.
“Lina” niliandika na kuruhusu. Nikasubiri
jibu. “Nashukuru kunipa lifti maana hizi adha
za daladala si mchezo”
“usijali mbona kawaida tu?” alinijibu.
Nilikuwa nilishamshukuru lakini nilirudia
maksudi ilia one najali.
“Poa. Naomba nikuulize kitu kama hutojali” mwanzo wa chombeza zangu
sasa.
“Eti unapenda utani?”
“Ndiyo. Maana nami najua kutania tena
usipoangaliwa waweza kulia kama mtoto
aliyeringishiwa nyonyo” alinijibu vyema. Nikavimba kichwa kikawa kama sim tank
la lita buku mbili.
“Vizuri. Kwani umelala?”
“Ndiyo nipo kitandani najibembeleza.”
“Mh! Unajibembeleza au
unabembelezwa?” Nilimhoji swali hilo maksudi tu ili tu nipate kumsogeza karibu
na utani wa kitandani.
“Ningekuwa nabembelezwa wala
usingeona nikijibu meseji zako kila
unapotuma.”
“Mh! Nisamehe katika hilo. Vipi unapendelea nguo ya rangi gani wakati
wa kusinzia usiku?”
“Pink na green.”
“Hapo ulipo umevaa rangi gani kati ya
hizo?”
“Green” “Natamani nikuone katika vazi hilo”
bahati mbaya kabla hajanijibu, simu
yangu ilizima chaji. Dah! Bahati mbaya
sikuwa nimepanga nyumba yenye
umeme kwamba niweke kwenye chaji
muda huohuo. Nikapitiwa na usingizi huku akili yangu ikiwa na matamanio ya
kundelea kuchat na Lina lakini nd’o hivyo
haikuwezekana.
**
Ni jumatatu majira ya saa nne asubuhi.
Nipo ndani ya gari la mzee Abas akinipeleka nyumbani kwake kwa ajili ya
kuifanya kazi yake kwa mkewe. Tulifika
mkewe akanionyesha uchangamfu wa
hali ya juu. Ni watu walioonekana kuwa
na maisha mazuri kutokana na mazingira
yao ya kimaisha. Baada ya kunifikisha, mzee Abas akatuaga na kuondoka hii
ikiwa ni baada ya kupigiwa simu na mtu
ambaye alionyesha kumhitaji haraka
iwezekanavyo. Nikatoa vifaa vyangu vya
kazi na kuanza kwa kumuosha kucha
mkewe. Nilipomaliza kumuosha kucha zake, nikaandaa rangi alizozitaka lakini
kabla sijampaka, simu yake ikaita.
Akainuka na kwenda kuichukua
chumbani. Kama dakika tatu alitumia
huko chumbani. Aliporudi akaniuliza, “hivi
mwanaume ni muoga kama mwanamke?” “Sina uhakika kwasababu hata usiku
mwanamke ndiye huomba kusindikizwa
nje tofauti na mwanaume ambaye
hutoka tu.”
ITAENDELEA..
No comments