Breaking News

SABABU VIFO VYA MAPEMA VYA WANAUME KWENYE NDOA

 

UTAFITI uliofanywa na Gazeti la Ijumaa umebaini kwamba kumekuwa na wimbi la vifo vya mapema zaidi ya wanaume kwenye ndoa kabla ya wanawake.

Utafiti huo ulibaini kwamba, kwa sasa idadi ya wanawake imekuwa ikiongezeka kila kukicha.

Katika kutafuta majibu ya kwa nini wajane ni wengi kuliko wagane (wanaume waliofiwa na wake zao), Gazeti la Ijumaa limezungumza na mtaalam wa saikolojia ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Chris Mauki ambaye amefunguka sababu zinazochangia hali hiyo.

“Kwanza ni umri mdogo wa kikomo cha maisha (life expectancy). Kama unafahamu hili jambo linaloitwa life expectancy utakubaliana na mimi kwamba umri wa mwanaume wa kuishi ni mdogo sana ukilinganisha na mke wake, hususan Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Kwa hiyo wanawake wanapewa nafasi kubwa ya kuishi muda mrefu kuliko waume zao.

“Pili ni ugumu katika kufunguka. Utakubaliana na mimi kwamba wanaume ni wagumu sana, tena sana kufunguka na kushirikisha mambo yao. Wao wako tayari wafe na tai shingoni wakijifanya hawaumii au hawasikii shida.

“Mkiwa na ishu kwenye ndoa, mkaitwa sehemu muyaongee, yeye kamwe hamumpati, anakwambia mambo yetu tutasuluhisha wenyewe wakati ndani yanamla na kummaliza.

“Tatu ni ishu ya ugumu wa wa kusamehe. Kusamehe siyo tu kwa faida ya anayesamehewa bali pia kwa afya ya wewe unayesamehe. Mzigo unaotokana na kusamehe huumiza sana mioyo ya wanaume, hata kama mara nyingine tunajifanya hatuna shida yoyote. Unaposamehe unaachilia mzigo mkubwa, wanaume wao ni wagumu sana kusamehe. Wako tayari wakubebe moyoni miaka na tena watakukumbusha uchungu wao kila wanapokuona. Hii inawala sana bila wao kujua.

“Nne ni tabia hatarishi. Wanaume wengi kwenye ndoa ndiyo wanaoongoza kushiriki tabia hatarishi kama vile ulevi, anasa, ngono holela na hii huwaweka karibu zaidi na jeneza kuliko wake zao waliowaacha nyumbani wakiwadanganya kuwa wako mkutanoni mkoani.

“Sababu ya tano ni ugumu wa kujali afya. Ni rahisi sana mwanaume kujisikia vibaya, lakini asiende hospitalini kuangalia afya, hata pale anapohimizwa kwenda bado anaweza kukwepa au kubisha au hata kusema kuwa ameshakwenda au ameshakunywa dawa kumbe mwongo. Wako pia ambao wanaweza kupewa dawa na wasizitumie.

“Sita ni msongo. Wanaume ndiyo wabebaji wakubwa wa shehena za msongo (stress) ingawa kwa nje wanajitahisi sana kuonesha kuwa mambo yako shwari wakati wanatafunwa ndani. Kaulize hospitalini, wanaokufa kwa presha ya kupanda au ya kushuka, stroke, kusimama kwa moyo, kupasuka kwa mishipa ya damu, matatizo ya mifupa au kuumwa sana kichwa ni jinsi gani?”

No comments