Breaking News

KWA WANAUME; SIKU WANAWAKE WAKIGUNDUA JAMBO HILI MMEKWISHA

 

Tumezichezea sana akili za wanawake. Tulianza kwa kuwaambia kuwa sisi ni bora zaidi yao. Wakanywea, wakawa wadogo wakiamini hakuna kiumbe duniani chenye ‘manguvu’ na ‘maakili’ ya ajabu zaidi yetu. Wakatusujudia, wakatuona ni miungu mtu, tena labda sio kutuona ni miungu mtu, bali mungu wa pili.
Na nguvu tuliyoitumia kuhakikisha hili linafanikiwa si ndogo. Tumetumia vitabu vya dini, vinavyosomeka kwamba Mungu mwenyezi baada ya kuumba kila kitu, akatuumba sisi wanaume na kutupa uwezo wa juu ambao hata malaika hawakuwahi kuwa nao, yaani kama ingekuwa enzi hizi za kiteknolojia tungesema Mungu katengeneza mashine yenye programu toleo jipya.
Kisha vitabu vya dini vikasogea sentensi kadhaa mbele ndipo neno mwanamke likajitokeza, sentensi zikasomeka kwamba mwanamke akatokea ubavuni mwa mwanaume yaani sawa na kusema bila mwanaume, kusingekuwa na mwanamke.
Ikaendelea mbele, ikaandikwa mwanamke akashawishiwa na shetani ili akamshawishi mwanaume wale tunda la mti wa kati na ikawa hivyo; hii ikamaanisha mwanamke alikuwa ni mdhaifu, tukaibeba na kuileta hadi leo mwaka 2019, na bado kuna wanawake kupitia sisi wanaamini wao ni wadhaifu.
Vitabu vikaendelea kuandika kuhusu mashujaa waliokuja kutetea ulimwengu, karibu asilimia 98 ya mashujaa wote walikuwa wanaume. Nuhu mwanaume, Musa mwanaume, Yesu (Isa bin Mariam) mwanaume, Yusufu mwanaume, Muhammad (S.A.W) mwanaume. Kisha asilimia kidogo tukawazungumzia wanawake, huku karibu asilimia 60 ya wanawake waliotajwa wakiwa ni wa upande mbaya.
Tukaweka vitabu vya dini pembeni, tukaja na historia. Tukawaambia kuhusu uhuru wa taifa kubwa kama Marekani, kisha tukawachorea michoro inayosema kuwa uliletwa ama kupiganiwa na wanaume kwa asilimia 98.
Uhuru wa Tanzania pia, wa Kenya, Uganda, Afrika Kusini na karibu wa kila taifa duniani ulipiganiwa na asilimia 98 ya wanaume. Kwa maana ya kwamba sisi ndiyo viumbe wenye nguvu au ni vipi?
Tukaja kwenye maendeleo ya dunia, tukasema kila kitu kiliigunduliwa na sisi wanaume. Gari, ndege, kompyuta, mashine ya kuchapisha magazeti, viatu hadi sufuria na vijiko, vyote ni sisi wanaume. Kwamba kwa kipindi hicho wanawake walikuwa wanafanya shughuli gani?
Matokeo ya yote hayo leo hii wanawake wanahangaika kulazimisha kufanana na sisi, kitu ambacho ni ujinga kwa kiasi fulani. Kwa sababu kama unataka kupiga hatua, kama unataka kuwa bora zaidi, hutakiwi kupambana kwa kiasi sawa na aliye bora. Unatakiwa kuhakikisha unakuwa bora zaidi ya aliyekuzidi ubora. Yaani kama wanawake wanataka kufanya mageuzi, wasihangaike kuwa kama sisi, au kuwa sawa na sisi, wahangaike kuwa bora zaidi ya sisi wanaume.
Tuwafundishe hili mabinti zetu, kuna mabadiliko yatakuja.

No comments