Breaking News

UHUSIANO WANGU KIMAPENZI NA HAMIDA - 1


IMEANDIKWA NA : JAMES JASON

*********************************************************************************

Simulizi : Uhusiano Wangu Kimapenzi Na Hamida
Sehemu Ya Kwanza (1)


xxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
...
"Hodiii!, hodi hodi humu ndani"

Nilibisha hodi huku nikigonga mlango kwa kutumia kipande cha chuma kilichoning'izwa maalum kwa ajili hiyo.

"Karibu, fungua mlango umeshindikwa tu"

Sauti nyororo ilisikika kutoka ndani.

"Starehe"

Nilijibu huku nikisukuma mlango mzito wa mbao ulio nakshiwa kwa ustadi mkubwa. (Neno 'starehe' enzi hizo ndio lilitumika kujibu pindi ubishapo hodi na kukaribishwa)

Nilipofungua mlango nikakutana na korido ndefu nyembamba (wakati huo iliitwa 'ukumbi' japo siyo kama kumbi tuzijuazo leo), pembeni kulia na kushoto kulikuwa milango, wa kushoto ulikuwa mpana ambapo ulikuwa wazi ukiwa umesitiriwa na pazia zuri jepesi lenye 'kuangaza' (transparent) la rangi nyeupe, upande wa kulia mlango ulikuwa umefungwa, na milango mingine mitatu pia ilikuwa imefungwa.

Mbele mwisho wa korido kulikuwa na mlango ambao ulikuwa wazi kiasi cha kuweza kuona nafasi kubwa iliyokuwepo na sehemu ya uzio wenyeji waliita uani (sikuhizi ukisema uani watu watajuwa ni maliwatoni)
************

"Karibu tupo huku varandani"
Ile sauti nyororo iliendelea kunikaribisha na sauti hiyo ilitokea upande ule wa pazia jepesi angavu ambapo nilivyoingia nikatambua kuwa pale palikuwa ndiyo sebuleni.

Kabla ya kuingia nilivua viatu vyangu (raba - Morogoro shoes), havikutoa harufu mbaya kwa kuwa ndiyo nimevivaa kwa mara ya kwanza baada ya kuvinunua, vilikiwa vya rangi ya bluu na soksi zangu nyeupe. Hapo mlangoni kulikuwa na viatu vya sandarusi vyenye ukubwa tofauti pea tatu... nikajuwa utaratibu wa kuingia humo ni pamoja na kuvua viatu.

Nilipekenyua pazia kulia na kushoto na kupiga hatua kuvuka kivingiti cha mlango na kukanyaga zulia zuri la manyoya manyoya.

Ndani niliwakuta wanawake wawili na mtoto mmoja mdogo wa chini ya miaka mitano. Wale wanawake mmoja alikuwa mwafrika, amejitanda vizuri ushungi huku akiwa ameshika ukili (alikuwa anasuka mkeka).

Wote walikuwa wamekaa chini na kuegemea mito midogo, hapakuwa na viti bali meza ndogo iliyo chinichini sana jirani na zulia.

Yule mwanamke wa pili alikuwa mweupe, asili ya Asia, na sikuweza kufahamu maramoja kama alikuwa Mwarabu ama Mhindi. Alikuwa anakoroga maji ya rangirangi akichanganya sukari na yale maji, bila shaka alikuwa anaandaa "ashkrim", watoto walikuwa wanaita hivyo. Zilikuwa zile "icecream" (malai) ambaozo maji huwekwa kwenye "kijikopo" kidogo kisha kuchomekwa kijiti cha chelewa ambapo maji yakiganda kile kijiti huwa ni sehemu ya kushika ashkrim hiyo.

"Karibu uketi"

Alisema yule mwanamke 'mwarabu' huku akiendelea na kazi yake.

Ndipo nikajuwa kuwa ile sauti nyororo ni ya huyo mama.

"HAMIDAAAA"

Aliita yule mama wa kiarabu.

Mara nikasikia sauti mlango fulani ukifunguliwa na kisha hatua za kivivu zikija upande wetu kutokea koridoni.

Pazia lilisogezwa pembeni akachungulia msichana aliye jitanda ushungi.

"Abee"
Yule binti aliitikia huku akimuangalia yule mama mkoroga malai.

"Hebu kamletee mgeni kinywaji"

Yule binti aliondoka bila kusema neno.

"Mzee Mjumbe nimemkuta?"

Niliuliza hivyo baada ya kuwasalimia kama ilivyo desturi na kujitambulisha.

"Tangia alivyoenda msikitini bado hajarudi, bila shaka atakuwa pale Shibam wanapocheza keram na zuna"

Alijibu yule mama huku ameinama akiendelea na kazi yake.
*************************

Michezo ya Keram, Zuna, Karata, Bao ilikuwa maarufu sana kwenye 'kijiwe' cha kahawa na tangawizi pale Shibam na sehemu nyingine jijini Dar es Salaam. Mambo na mipango mbalimbali ilijadiliwa hapo ikiwemo siasa, michezo nk.

Mara yule binti alirudi huku ameshika magi iliyojaa sharubati na mkono wa kushoto ameshika bilauli ya bati.

Alimimina ile togwa kwenye ile bilauli mbele yangu kisha akanipatia. Ilikuwa togwa ya mtama uliokobolewa na kutengenezwa kwa ustadi mkubwa.

Maeneo ya FAYA (fire brigade) hivi sasa, zamani palikuwa na mti wa muembe mkubwa ambapo palikuwa maarufu sana kwa biashara ya togwa hadi eneo hilo likapewa jina la "mwembe togwa"

Pia haikuwa ajabu kukuta sinia yenye maji iliyowekwa chupa za 'fanta' ndani mkiwa na togwa, imezibwa na kipande cha gazeti iliyokunjwa vema kwenye kila chupa, wengine waliweka chupa moja tu ama stuli iliyofunikwa kawa bila kitu ndani, wateja hutambua moja kwa moja kwamba hapo kuna biashara fulani.
**********************

Niliipokea ile bilauli na kuigigida (kuinywa kwa haraka) kwa nilikiwa nataka niondoke niwahi kupeleka ujumbe sehemu nyingine kwa kuwa hapo tayari niliwaachia moja ya barua nilizokuwa nazo.

Nilikuwa nina karatasi kadhaa (barua) za kuwasambazia wajumbe wa nyumba 'kumi kumi' (waliitwa hivyo) kutoka kwa Katibu Kata, Kata ya Magomeni...

Niliwaaga wale wenyeji mle sebuleni na kuanza kuondoka. Yule binti naye akachukuwa ile bilauli pekee na kuacha magi yenye togwa iliyobakia pale sebuleni...
***********

Wakati navaa viatu pale koridoni, Hamida (siyo jina lake halisi) naye akawa anakuja kutoka uani (siyo maliwatoni) huku ameshika bilauli nne mkononi...

Nikawa namuangalia huku nikiwa nafunga kamba za viatu. Mara ghafla mtandio ukateleza akabaki kichwa wazi...

Moyo ulinilipuka paa! Kwa kumuona Hamida vizuri waziwazi...

Aliinama haraka haraka na kuchukuwa mtandio wake lakini kwa bahati mbaya tena zile bilauli zikamponyoka na kuanguka sakafuni...

=
=
=
.......
****
Hivi ndivyo nilivyokutana na Hamida wangu...



Kabila langu ni Taturu, baba yangu alibahatika kufanya kazi na Padri fulani mkoa wa Singida, hivyo masikio yangu yalinusurika kutobolewa, mimi pamoja na mdogo wangu niliyemuachia ziwa.

Miezi kadhaa nikiwa nimerudi nchini kutoka masomoni Ulaya, nikiwa mwajiriwa wa RTC maarufu kama UGAWAJI enzi hizo (siyo TRC), nilimtafuta Rose (wa Lindi; stori yake ipo kwenye uzi wa kula tunda kimasihara), Rozi hakujibu barua zangu tangia nilipo kuwa Ulaya. Miaka mitano ilikuwa imeshapita sasa.

=

Rose nilimuacha Lindi na kurudi Dar es Salaam baada ya kuwa naye Lindi kwa uhusiano wa mapenzi motomoto ya miezi miwili. Nikiwa Dar tulikuwa tunawasiliana kama kawaida lakini sikupata bahati ya kuonana naye ana kwa ana hadi leo hii ninapoandika haya.

=

Nilikata tamaa ya kuendelea kumtafuta, kazi yangu nayo ilichangia kwa kuwa nilikuwa bize mno hususani baada ya kurudi masomoni na kupandishwa cheo...

Labda mchumba wake aliendeleza uhusiano wao na kumuoa, hivyo aliamua kukata mawasiliano, hii ndiyo dhana kuu niliyobaki nayo, nahisi mtoto wake wa kwanza ni damu yangu.
************************

James mimi nilikuwa "kiwembe" sana kabla ya kukutana na Rose, umri wa kuoa ulikuwa umeshafika hivyo nilidhani kwake Rose ningehitimisha useja.

Baada ya kukata tamaa niliamua kuendeleza wimbi la 'ubazazi', kutembea na kila binti mrembo niliyemtaka...

Uingereza 'sikutembea' hovyo, nilikuwa na girl friend mmoja tu mwanchuo mwenzangu aliyetokea Hispania, Sue Parterson. Miss Sue ndiye aliyenipatia kitabu "Frech Sex Art Manners" kilichoandikwa na G. Valensin, nilijifunza mengi lakini uhusiano wangu na binti Paterson haukuwa wa malengo ya mbali, hivyo niliachana naye miaka miwili kabla ya kurudi nchini (nilidumu yaye kwa miaka miwili na miezi tisa hivi) ambapo nilienda Kaskazini zaidi kuchukuwa post graduate diploma fulani.

Enzi hizo kabla ya kwenda Ulaya hususani Uingereza, kulikuwa na utaratibu wa kupata semina fupi pale British Council, kwa ajili ya kuwaweka sawa kukabiliana na mazingira ya huko. Nakumbuka pamoja na mambo mengine tulifundishwa kufunga tai  (japo nilikuwa najuwa kabla)

Nilivyorudi Tanzania, nikapewa nafasi nzuri katika RTC (Regional Trading Company), nikatumia kufahamika kwangu na umuhimu wangu kujipatia mabinti warembo kila uchao hadi siku hiyo moyo uliponilipuka kwa kumuona Hamida.
*************************************

Makatibu Kata walitusaidia sana katika kazi zetu, nikazoeana na Katibu kata mmoja ambaye alikuwa Kata ya Magomeni.

Kulikuwa na mkutano uliandaliwa kati ya Uongozi wa Kata na wajumbe wa nyumba kumi kumi kuhusiana na hali ya upatikanaji wa bidhaa katika mkoa.

Nchi ilikuwa imetoka vitani, (Tanzania vs Uganda), hali ya uchumi ilikuwa imeyumba hivyo wajumbe walitakiwa kuwaandaa waananchi katika mashina yao kukabiliana na hali inayoanza kujitokeza.

Mzee Katibu Kata rafiki yangu nilipomtembelea afisini kwake, (nyuma ya Hotel Travertine hivi sasa) ndipo akaniomba nimsambazie barua kwa baadhi ya wajumbe Magomeni Mapipa; alikuwa hajisikii vizuri (alikuwa ana homa)

Magomeni Mapipa enzi hizo palikuwa maarufu sana, hapo ndipo kulikuwa na U-turn kubwa kwa ajili ya magari aina ya 'Ikarus' kugeuzia.

Mabasi haya pamoja na mabasi mengine yalikuwa yanamilikiwa na Shirika la UDA (Usafiri Dar es Salaam) ambapo walikuwa na mabasi yaliyotengenezwa na kampuni mbalimbali ikiwemo Mercides Benz (German), Isuzu (Japan), Ikarus (Hungary) nk.

Wanafunzi walikuwa wanapenda sana kupanda Ikarus, na waliyaita "ikarus kumbakumba" maana likija moja lilikuwa linapakia abiria wengi kwa mara moja. Mfano wake ni kama haya mabasi ya Kichina ya BRT yale marefu.
*****************************

Wakati nimechuchumaa nafunga viatu kamba huku nikimuangalia Hamida akiwa ameinama kuokota mtandio wake pamoja na bilauli zile, yule mama mwenye sauti nyororo nikimsikia akisema " Kwema huko?, taratibu mnatushtua na presha hizi..."

"Ziliniponyoka, ngoja nikazisuuze tena nizilete"

Hamida alijibu, nikaisikia sauti yake nyororo akiongea sentesi nzima.

Maa shaa Allah kumbe naye ana sauti kama ya yule mama Mwarabu.

"Kwaheri Hamida"

Nilijikuta nimeropoka huku nikirudi kinyumenyume kuelekea mlango wa kutokea nje. Hamida hakujibu kitu, aliinama na kugeuka akaelekea uani (siyo maliwatoni), mtandio alijifunika kichwani lakini kwa kuutupia tu.

Niligeuka na kuvuta mlango kwa ndani na kutoka nje.
***********

Mzee Burhani ni mjumbe wa nyumba kumi katika mtaa huo nilipotoka, ni mzee kwenye hekima na mcheshi sana, muislamu safi na mwenye kuipenda familia yake na jamii aiongozayo kwa ujumla.

"Salama leko"

Nilisalimia kama waislamu wanavyosalimia, waliitikia lakini mzee mmoja wa makamo akaniambia, wewe James inabidi ujifunze kusalimia vizuri...

Hatusemi salama leko bali tunasema Assalaam aleikum. Pale pale nikarudia

"Assalaam aleikum"
Wakaitikia tena kwa wingi.

"Inabidi usilimu kijana."
Mzee Burhani alidakia.

"Hahhaha" nilicheka, kisha nikamwambia kuwa ule ulikuwa ni 'mguu wake'

Kwakuwa haikuwa siri nilimueleza kuwa nilipitia nyumbani kwake na kuacha barua na kumpa yaliyo ndani kwa ufupi, kisha nami nikajisogeza kwenye benchi nikaketi huku nikiangalia wanavyocheza keram.


Pale Shibam kwenye 'kijiwe cha kahawa' nilikaa dakika chache tu, 'niliwapiga' raund moja ya tangawizi wale wazee waliokuwepo pale kisha nikaaga na kuondoka kumalizia kusambaza zile barua nilizobakinazo.

Nilinyonga batavus yangu (aina fulani ya motorcycle) na kuwaka nikaendelea mitaa mingine.

Kabla ya machweo nilikuwa nimeshamaliza kazi niliyopewa na 'Mzee Katibu Kata', hivyo nilielekea moja kwa moja nyumbani.

Hapo Dar nilikuwa naishi kwenye nyumba za Shirika la nyumba (NHC) zilizokuwepo Magomeni Mapipa (jirani na Tanesco Magomeni), zilikuwa nyumba bora sana enzi hizo. Miaka mitano nyuma nilikuwa nakaa 'kota' zilizokuwepo jirani na kituo cha afya Magomeni Mapipa (hospitali)

Ilikuwa siku ya Ijumaa, jua limezama nami nipo ndani kwangu nikizinyoosha (kupiga pasi) nguo la kutokea usiku huo pamoja na nguo nyingine...

Ilikuwa ni nadra sana kwa vijana wa kariba yangu ifikapo mwisho wa juma (weekend) kuwepo nyumbani baina ya saa mbili na nusu usiku hadi saa sita usiku (wengine hadi alfajiri)

Nilikuwa mpenzi sana wa muziki wa dansi hususani DDC Mlimani Park Orchestra, hivyo kila jumamosi nilikuwa sikosi pale DDC Kariakoo, Magomeni Kondoa ama Lango la jiji.

Ijumaa hii nilipanga kwenda sinema, (Empire). zama hizo kumbi za sinema ndiyo zilikuwa kimbilio letu kwa ajili ya kuburudika na filamu mbalimbali.

Starehe za sinema miaka hiyo kwa Dar es Salaam kimbilio la 'wanyonge' lilikuwa pale Oysterbay, Drive-in Cinema, ambapo screen ilikuwa kubwa na imewekwa juu sana kiasi cha kuweza kuonekana na watu wote hata walio nje ya ukumbi, hivyo wasiokuwa na uwezo wa kulipia kuingia (na magari yao), walikaa nje kwenye majani mafupi ama vumbini, wakifuatilia filamu, mbu nao walipata lishe ya kutosha.

Kulikuwa na kituo cha daladala eneo la Drive-in Cinema baadaye makondakta wa madaladala wakawa wanafupisha kuita jina lote na kupaita "drai"

Cameo, Empire, Empress, Avalon na Odeon cinema ni baadhi ya kumbi za sinema zilizokiwa maarufu sana Dar enzi hizo. Ratiba yangu wiki hiyo ilikuwa ijumaa kwenda sinema (Empire), jumamosi DDC kariakoo na jumapili kutulia nyumbani baada ya ibada kwa ajili ya maandalizi ya jumatatu kazini.
****************

Saa mbili kasoro robo (tuliita saa mbili kasorobo) nilikuwa tayari nimemaliza kazi muhimu nikafungulia redio (RTD) kipindi pendwa cha michezo, nakumbuka siku hiyo kilitangazwa na Julius Nyaisanga (R.I.P)

Nilibahatika pamoja na vitu vingine, kurudi na radio cassete (music system) kutoka Ulaya. Kabla ya hapo nilikuwa na radio cassete ya kawaifa pamoja na 'player ya santuri' (turntable). Kurudi na music system enzi hizo ilikuwa ni fahari sana...

Saa mbili na robo hivi baada ya kusikiliza taarifa ya habari na mazungumzo baada ya habari, nilikuwa tayari kutoka.

Nilichukuwa pikipiki yangu (batavuz) na kuelekea Butiama Restaurant kupata pilau safi ya moto kabla ya kuelekea mjini maeneo ya posta mpya (mtaa wa maktaba) ukumbi wa Empire kuangalia filamu ya Kihindi iitwayo Kurbaan. (Ile kurbaan ya zamani maana sikuhizi nasikia kuna kurbaan mpya na kurbaaniyan)

Filamu hiyo ilitangazwa kwenye kurasa za magazeti maarufu ya enzi hizo, pamoja na mabandiko (posters) kwenye ubao wa matangazo wa Empire.

Filamu nilizianza kuzipenda tangia nipo shule ya kati (middle school), kuna wamisionari walikuwa wanatuletea filamu ya maigizo ya maisha ya Yesu, na kule kijijini kwetu kuna wakati landrover fulani ilikuja na kutuonesha filamu ya namna ya ukulima bora, sikumbuki hata ilikuwa taasisi gani. Kuna baadhi ya viongozi na watu maarufu nilianza kuwaona kupitia filamu hiyo tuliyoletewa kijijini kwetu.
*************************************

Trela (trailer) ilikuwa imeanza tangia saa mbili, mie nilifika saa tatu kasoro kidogo tu, Saa tatu kamili filamu ingeanza.

Waonesha filamu enzi hizo walitumia projector kubwa sana zenye kutumia 'film' (mkanda kwenye magurudumu) kama kitunzia / chanzo cha picha. Mikwaruzo kwenye sauti na picha na chengachenga zilikuwa ni sehemu ya burudani pia kwani hakukuwa na namna bora zaidi wakati huo.

Nikakata tikiti (tiket / ticket) na kuruhusiwa kuingia ndani. Nikapanda ngazi fasta na kuangaza sehemu iliyokuwa wazi, nikapaona nikaenda kuketi; filamu ikaanza na wote tulianza kufuatilia.
***************************

Katika sinema za Kihindi, pamoja na uzuri wa maudhui, lakini pia nilikuwa napenda nyimbo zao. Lugha ilikuwa inatumika ya Kihindi, japo sehemu chache walichanganya na Kiigereza, hakukuwa na sub-titles za kutusaidia, bali kulikuwa na 'spoilers' ukumbini 'much know' sana na kuanza kuhadithia (uongo ulikuwa mwingi sana), usiombee uwe jirani nao! lakini bado tulikuwa tunafurahia.

Katika filamu hiyo pia kulikuwa na nyimbo nyingi, lakini kuna songi (wimbo) mmoja uliniteka hisia sana.

Natamani niwaimbie hapa lakini nimeusahau, ila nakumbuka 'tone' yake.

Kuna Mwimbaji mmoja maarufu sana wa taarabu (R.I.P) aliuiga kwa kuweka maneno ya Kiswahili, aliuta LEILA

 Leila Leila Leila, Ewe wangu Leila, kila mtu hapa, akupenda wewe..

Huo ndio wimbo uliniteka sana kiasi cha kunifanya nimkumbuke Hamida...

Wimbo ulikuwa unaimbwa kwa Kihindi, lakini ulikuwa una hisia sana, nilijikuta nimetumbua macho kuangalia screen lakini mawazo yote ni kwa Hamida..., nitampataje Hamida! Kwa uzuri wake, bila shaka kila mtu anampende Hamida (niliwaza)

=

Kulikuwa na Mapumziko mafupi kwenye filamu hizo (half-time), waoneshaji walikuwa wana rewind mikanda na kuandaa mkanda mwingine kwa ajili ya muendelezo, pia kuwapa nafasi watazamaji kunyoosha miguu na kwenda maliwatoni, kununua viburudisho (bisi zikiwemo ), pia kutoa nafasi ya baadhi ya watazamaji kufuta machozi ama kurudi katika hali zao za kawaida maana filamu zilikuwa zinateka hisia haswa vile vile simema yenyewe ilikuwa ni ndefu (long play), ilitumia dakika 90 kufikia halftime.

Wakati wa halftime, nilimpata dada mmoja na kumshawishi tukae pamoja kwa kuwa siti niliyopata palikuwa na nafasi nne ama tano wazi, ilikuwa siti za katikati nyuma kabisa ambapo juu yake kulikuwa kunapita ule mwanga mkali ya projector.

Alikubali baada ya ushawishi mkubwa, alikuwa yeye na rafiki zake wawili wote wakitokea maeneo ya Upanga. Tukanunua bisi (pop-corn) na chingamu (chewing gum) na kurudi ukumbini.

Kipindi cha pili kiliendelea, na tuliendelea kufurahia falamu hadi mwisho. Ilikuwa saa sita na robo hivi usiku tulipotoka ukumbini.

Niliwalipia taksi (co-cabs) wale rafiki zake, siye kwa kutumia kibatavuzi hao tukawa tunawafuata kwa nyuma kuelekea makutano ya barabara ya maktaba na bibi titi (Ali Hassan Mwinyi Rd. iliitwa hivyo kabla), walikunja kulia kufuata barabara hiyo hadi mbele kidogo ya Redcross na kukunja kushoto...

Wao walisimama nyumba fulani nasi tukapitiliza kuitafuta barabara ya Umoja wa mataifa, tukakunja kushoto ili kuelekea faya ili tuikamate barabara ya Morogoro.

Saa saba na dakika chache tulikuwa tayari tumefika mtaani kwangu. Palikuwa kimya sana, kulikuwa na kile 'kibaridi cha Dar cha usiku', nikafungua mlango, nikaingiza pikipiki na kumkaribisha dada niliyekuja naye.

"karibu sana Egline" (siyo jina lake halisi), nilimkaribisha.

Egline alikuwa mtoto wa mwansheria fulani ambaye wiki hiyo alikuwa safarini Nairobi, hivyo siku hiyo walipata fursa nzuri ya kujivinjari walipotaka bila kikwazo, mama yao hakuwa "noma". Wale rafiki zake kumbe ni watoto wa mama yao mkubwa, walikuja kumtembelea mama yao mdogo kutokea Same - Kilimanjaro.

Ndani nilikuwa nina vinywaji kwenye jokofu dogo (friji), kulikuwa kuna fanta, double cola, pilsner na brandy (Cognac ya Ufaransa) ambayo ilikuwa kwenye kabati lingine.
*******

Tuliamka saa tatu asubuhi baada ya kengele ya kwenye saa kubwa ya mezani (alarm clock) kulia....

Baada ya staftahi nilimchukulia teksi kwenda kwao...

Kulala na Egline ilikuwa ni starehe ya usiku mmoja tu. Usiku ule tulifaidi vinywaji na ngono kiasi, sikuwa vizuri kutokana na mawazo juu ya Hamida.

Naanzaje kumpata Hamida? Nazidi kujiuliza, nilitamani kumuoa kabisa kwa kuwa alikuwa na sifa zote za kuwa mke bora (kwa mujibu wa moyo wangu)

Mimi ni mfuasi wa Roman Catholic, niliyependwa sana na Padri Petro aliyekuwa anafanya kazi na baba yangu Mission ya Chemchem Iramba Singida, Padri ambaye ndiye aliyenisaidia sana katika masomo yangu kabla ya middle school na wakati wa middle school. Niliwaza.

Mimi, ambaye kabila langu ni Mtaturu (siyo Mnyaturu), Mwafrika mweusi, naanzaje kumpata Hamida. Hamida ambaye hata hajui kwamba kuna James anayemtaka, sembuse (seuze) kumuoa.

Mawazo yalinijaa hadi nikapitiwa na usingizi nikiwa sebuleni kwenye makochi. Nilikuja kushtuka ikiwa tayari saa tisa alasiri, njaa inauma.

Nikaenda kujimwagia maji, nikavaa kisha nikatoka kuelekea Shibamu.
*****************************


Bourne ni babu yake James, mzee wa Kitaturu (kabila linalofanana na Wamang'ati), wahamiaji kutoka kandokando ya ziwa Eyas, Manyara hadi kuja Iramba katika harakati za kutafuta maisha bora.

Jason, mtoto wa saba kati ya watoto kumi na mmoja wa mzee Bourne, alibahatika kufanya kazi na Padre (Padri) kwenye Mission fulani iliyopo Chemchem - Iramba. James ni mtoto wa kiume wa kwanza katika uzao wa Jason ambaye alikuwa na watoto watano, yaani Dada zake James wawili walianza kuzaliwa, kisha James, halafu mdogo wake James wa kiume na kitinda mimba alikuwa wa kike.

Elimu ya madarasani katika maisha ya wawindaji na wafugaji haikuwa kipaumbele, lakini kwa bahati nzuri kutokana na bidii ya mzee Jason, yule padri aliahidi kumsaidia watoto wake wapate elimu. Elimu hiyo ilimfanya James afike Shule ya Sekondari Kibaha na kukaa huko miezi 10 na wiki mbili bila kurudi Kijijini. James anasimulia safari yake...
****************************************

Mwaka 1961 nikiwa nina miaka saba, dada zangu waliandikishwa kusoma shule ya msingi Chemchem, nami katika msafara huo niliwasindikiza tukiambatana na baba yetu Jason. Dada zangu wote walipimwa kwa kujishika masikio kwa kuzungusha mkono mmoja kichwani na kuweza kuyagusa masikio yao, wakaandikishwa. Kiumri dada zangu hao wakubwa wamepishana miezi kumi na minane tu kuzaliwa. Dada yangu aliyeniachia ziwa tumepishana miaka miwili.

Hamu ya kujiunga shule nami inanijia, nilitamani nami nivae sare zile za shule.

Nikajipeleka kwa Mwalimu muandikishaji, akaniambia shika sikio, aaah wapi! Sikulifikia, nikafanya hila na kulishika lakini aligundua na kuniambia wewe uje mwakani
=
=
=

Mwaka uliofuata nilimsumbua sana baba anipeleke kuniandikisha shule, hatimaye alifanya hivyo lakini kwa bahati mbaya muandikishaji yule yule alinikataa kwa kusema bado sijafikia 'umri', na kweli siku hiyo pia sikuweza 'kugusa sikio'.
**********************************

Nilishachoka kazi ya kuchunga ng'ombe mbuzi na kondoo, maisha ya kupigana chenga na nyoka wa porini ama kupambana nao, maisha ya kula ugali mgumu asubuhi kwa mlenda pori na kushinda bila kula hadi jua lizame, maisha ya kujitafutia matunda ya porini na kula kufidia pengo la njaa, maisha ya kufunga 'lubega' (kuvaa shuka moja jeusi kama kaniki), maisha ya kupiga miluzi na kelele kudhibiti mifugo isiingie kwenye mashamba ya watu... Nilikuwa nimechoka kwa kuwa sasa kazi ya uchungaji ilinielemea, dada zangu muda mwingi walikuwa shuleni.

Sikujali "mzigo" utamuelemea nani, nikamwambia baba kuwa nitaenda shuleni vivyo hivyo.

Siku iliyofuata nilienda kinyemela na kuingia darasa la kwanza na kukaa nyuma kabisa kwenye sakafu kama wanafunzi wengine huku nikiwa nimevaa lubega...

Huku nyuma baba alitafuta utaratibu wa ng'ombe kwenda machungani kwa kuchanganya na ng'ombe za jirani, pia alimuelezea Padri juu ya maamuzi niliyofanya. Padri alimuambia aniache waone itakuwaje.

Darasani siku hiyo sikuwa najibu chochote, lakini masomo nilikuwa nayaelewa vizuri. Siku ya pili tena nilienda shuleni, Mwalimu waa hesabu alikuwa anapenda kuuliza maswali mara kwa mara, nakumbuka kuna swali wanafunzi wenzangu liliwashinda mie nikanyoosha mkono na kujibu kwa usahihi. Mwalimu alifurahi sana.

Mwalimu wa hati naye alipoingia, wakati anakagua vibao vyetu vya kuandikia (tulianza kuandika kwenye vibao vyeusi vidogo, tulikuwa tunapewa chaki), alikuta nimeumba vizuri herufi zote alizotufundisha. Akachukuwa ubao wangu na kuondoka nao....

Sijui nini kiliendelea kwenye afisi (ofisi) za walimu lakini niliona siku chache baadaye baba ameniletea kaptula na shati (sare za shule), nilifurahi sana.

Wakati huo, siyo wazazi wote waliweza kuwa na sare za shule, kwa msaada wa Padri Petro mambo yalienda vizuri (Petro siyo jina halisi, na majina yote kwenye stori hii si halisi isipokuwa majina machache sana kwa sababu maalum)
****************************

Ilipofika wakati wa majaribio ya nusu muhula, nilipata masomo yote mia kwa mia na kuwa mwanafunzi wa pili darsani nikitanguliwa na Abel ambaye alikuwa wa kwanza. Muda wote wakati nahudhuria darasani nilikuwa siendi mstarini wala kufuata taratibu zingine za shule, wala jina langu halikuwemo kwenye 'rejista' ya mahudhurio.

Lakini baada ya matokeo hayo, jina langu likaanza kuitwa darasani, Padri aliniletea suruali ya mtumba aina ya jeans (rangi ya bluu), ilikuwa kama 'ovaroli' lakini isiyo na mikono, mikanda yake nyuma inaweka alama ya 'X' na mbele kifuati inaziba. Japo ilikuwa ndefu kiasi lakini niliifurahia sana.
******************************************

Baba alikuwa akifanya kazi ya kumsaidia Padri katika kampeni yake ya kupanda miti (alikuwa anatunza bustani ya vitalu)

Umbali kutoka kwenye 'boma' yetu hadi shuleni ni parefu kiasi cha kutembea saa nzima njiani. Tulikuwa tunakaa mbugani baina ya mto Sibiti na Misheni ya Chemchem. Nyumba zetu zetu zilikuwa tatu, nyumba za miti zilizokandikwa kwa matope yaliyochanganywa na kinyesi cha ng'ombe, sakafu nayo imesilibwa vizuri kwa "nilu" ya kinyesi cha ng'ombe, vitanda ni miti ilishoshindiliwa chini vizuri (matendegu) kisha juu kuwambwa ngozi ya ng'ombe. Nyumba kuu aliishi baba, mama na wadogo zangu, nyingine alikuwa anaishi babu, bibi alishafariki nikiwa mdogo, na nyumba nyingine nilikuwa nakaa mimi na dada zangu. Nyumba zote zilikuwa zimeezekwa kwa kuwekwa miti na kujaza udongo (tembe), kando ya nyumba hizi ndipo kulikuwa na zizi la mifugo ambalo uzio wake ulikuwa majani ya miba.
Tulishazoea maisha hayo na umbali kutoka boma hadi boma palikuwa parefu sana.
*****************************************

Niliendelea na msomo na kufanya vizuri darasa na nne mwaka 1965 na kuchaguliwa kujiunga na midle school Tabora.

Januari 1965, Padri Petro alinifuata nyumbani kwa ajili ya kunipeleka Kinampanda kwa usafiri wa pikipiki (BMW), tulikuwa tunaiita tukutuku, ina shafti ya mfumo wa upeleshi (propeler shaft) na kitu kama maboksi mawili nyuma kila upande ambayo yalikuwa hayaondolewi muda wote. Ilikuwa pikipiki ya rangi ya kijani iliyoiva.

Kwa mara ya kwanza nilipanda pikipiki (na chombo cha moto kwa ujumla), kabla ya hapo nilikuwa napanda mikokoteni ya kuvutwa na ng'ombe kwenye harakati za kupeleka mazao mnadani ama mambo ya shambani, ujenzi, na usafirishaji wa vitu vingine.
********

Niliagwa vizuri na familia, mama yangu alinihusia niwe na tabia njema na kusoma kwa bidii, dada zangu walikuwa wananipungia mikono huku machozi yakiwalengalenga, Babu alisemasema maneno yake (Kitaturu cha ndani - 'kubonga' ) ambayo sikuwa nayaelewa kisha akaniambia "nenda salama mjukuu waku na Mungu akusaidie", mdogo wangu wa kiume niliyemuachia ziwa alinipa mkono na kunitakia safari njema, wala hakuniangalia sana, aliingia ndani.

Nikiwa nimemshikila Padri vyema, huku nimevaa fulana na jeans yangu ambayo sasa ilikuwa inanitosha vyema, niliangalia nyuma na kuona boma letu na familia wakiwa bado wananipungia mikono, niliwapungia nami kisha nikamshikilia vizuri Padri.

Tukafika Chemchem 'Mission' akaniacha nje kwa muda, akaingia afisini kwake, na baada ya muda akaniletea peremende (pipi fulani hivi ) na kuniambia niendelee kumsubiri.

Alivyorudi tuliendelea na safari, tulivuka mito mikubwa miwili ambayo kwa wakati huo haikuwa na maji yanayotembea (mito ile hupitisha maji kwa wingi sana wakati wa mvua lakini ndani ya siku ne au tano maji huisha. Wanakijiji hutumia maji hayo kwa matumizi mbalimbali. Maji yakikauka mtoni, wanakijiji huchimba kwa kutumia mabakuli ya bati ama mabakuli ya kienyeji (wanaita 'vipeyu'), kiasi cha futi moja ama mbili kwenda chini unakutana na maji, ila kiangazi unaweza kuchimba hadi meta (mita) moja na nusu. Lakini sisi kule mbugani unafuu tulikuwa tunaupata wakati wa mvua tu, nyakati za kiangazi ilibidi kutumia mifugo na mkokoteni kufuata maji sehemu za mbali.

Maisha yalikuwa yenye changamoto nyingi, msimu wa njaa kali nikiwa daresa la nne tulikuwa "tunashindia" viazi vilivyo menywa na kukatwa slesi kisha kukaushwa juani, mengine huchemshwa kwanza (makela / chepe, mapalage, matobolwa), kupopoa mabuyu kisha unga wake kutengeneza 'uji' ilikuwa kawaida, kula matunda ya "mihama" (palm), ambayo tembo huyapenda sana kuyala, ilikuwa ndio pona yetu machungani. Mizizi ya mimea fulani (ilonge) hizi nayo ilituokoa nyakati hizo, matunda pori aina mbalimbali yalitusaidia, hususani 'mitogo' ambayo ilikuwa na sukari na unafaguna kama bigijii (big G)
***********************************

Safari iliendelea tukapita kijiji cha Ibaga, Mkalama, Gumanga kisha tukaacha njia ya kuelekea Nduguti na kushika njia ya kulia na kuukabili mlima mrefu ambapo tulipoupandisha dakika chache baadaye tukafika Kinampanda (Mission), tulipokelewa na masista wa Kilatino (Latin American nuns) (nilijuwa baadaye sana)

Nilioneshwa ukarimu mkubwa sana pale, chakula kizuri na kuoneshwa chumba cha kupumzika. Padri Petro baadaye alikuja kunijulisha kuwa safari nyingine itakuwa kesho kuelekea Singida mjini kisha Itigi ambapo nitapanda treni kuelekea Tabora.
******************************************

Kesho yake majira ya saa nne hivi, mimi pamoja na masista kadhaa tulielekezwa tupande gari fulani hivi (baadaye sana nilikuja kulifahamu kuwa ni UNIMOG - Mercedes Benz iliyotengenezwa "under licence" kutoka Argentina. Ilikuwa na rangi fulani hivi khaki iliyopauka.

Tulikwea nyuma (kwenye bodi) na kukaa kwa mtindo wa kuangaliana, kijana mdogo nikiwa peke yangu, masista wa kilatino walikuwa wengi na wachache walikuwa waafrika.

Safari ilianza, Padri Petro tulimuacha hapo, kabla ya safari alinipatia sanduku dogo ambalo aliniambia ameniwekea baadhi ya mahitaji yangu muhimu. Nilimpungia mkono wa kumuaga naye alifanya hivyo.
******************************************

Safari iliendelea hadi nilipoanza kuona 'bwawa' kubwa, ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuona bwawa la namna hiyo ambapo baadaye masista waliniambia lile ni ziwa dogo liitwalo Singidani.

Mji wa Singida ukaanza kuonekana vyema na nilifurahi moyoni kuona nyumba nyingi pamoja na nyingi zikiwa zimeezekwa bati.

Tukapita Bomani kisha tukaelekea Singida mjini, kuna sehemu tulisimama kidogo lakini alishuka "mzungu" mmoja aliyekaa mbele (hakuwa dereva), akaingia kwenye jengo fulani kisha baada ya muda mchache alirudi tuaendelea na safari kuelekea Itigi.

Barabara haikuwa rafiki, tuliwasili Itigi majira ya jioni, na wale masista wote walipanda treni ya abiria iliyotoka Mwanza kuelekea Dar.

Mie nikabaki na yule mzungu, baadaye aliniletea chakula na muda mfupi baada ya kula nilipatwa na usingizi...

Niliamshwa alfajiri wakati treni nyingine ya abiria iliyotoka Dar kuelekea Mwanza ilipokuwa inakaribia kuwasili. Muda wote wa kusubiri tulikuwa eneo la kupumzikia aribia pale Itigi Railway station.
********************************

Yule mzungu alilichukuwa blangeti (blanket) alilonifukika nilipopitiwa na usingizi, na kuniambia nijiweke tayari huku akinikabidhi tikiti (tiketi) yangu. Ni kadi fulani hivi ndogo na ngumu sana rangi kama ya pinki.

Nikasikia sauti honi kali, 'bila shaka itakuwa ndiyo treni hiyo' niliwaza. Kweli muda si mrefu treni ikaanza kuonekana, ikapitiliza tulipokuwa tumesimama...

"Kumbe ndefu hivi!" Nikishangaa kwa sauti...

Pamoja na kupitiliza lakini bado niliona urefu uliobakia kushoto kwangu.

Haraka haraka nikaingia kwenye treni, behewa nliloingia lilikuwa limejaa sana (daraja la tatu), sikupata hata nafasi ya kumpungia mkono yule mzungu aliyenisindikiza.

Begi nilikuwa nimeweka kichwani na kulishikilia kwa mkono mmoja huku nikihangaika kutafuta nafasi ya kuliweka. Tulikuwa tumejaa sana kiasi kwamba hata kupiga hatua kusogea ilikuwa ni kwa shida.

Baada ya dakika chache nikasikia tena zile honi kali, safari hii zikiwa kali zaidi, ilipolia honi kubwa mara ya pili nikasikia psiiiiiiiiiiiiiii, chwaaaa! Nikayumba sana, kumbe ndio ilikuwa imeanza kuondoka.

Bahati nzuri baba mmoja akanionea huruma akaniambia shusha begi lete hapa, nikampatia, akalisokomeza chini ya siti aliyokaa.

Uhuuuu! Nilipata nafuu, nikamshukuru na nikaanza mchakato wa kusimama vizuri.
******

Safari iliendelea, huku nikisikia sauti "mziki" wa aina yake kwa jinsi gurudumu za treni zinavyopita kwenye reli. (Kata mti panda miti, kata mti panda miti..) Sauti hiyo iliendelea kusikika japo si kwa maneno bali hisia.

Kufika sehemu fulani, kukawa na utulivu mkubwa sana ndani ya behewa, treni nayo ilikuwa inaenda taratibu kuliko mwanzo...

"Sekenke hiyo..." Alisikia kijana mmoja akisema. Mie hata sielewi maana yake nini, lakini baadaye kidogo treni ilirejea kwenye mwendo wake wa kawaida.

Baadhi ya abiria walikuwa wanatembea kwenda mabehewa mengine, wengine walipita wakielekea msalani, kuna muda alipita mtu mwenye sare (siyo polisi) alikuwa anagonganisha vitu kama vijiko, nilisikia pia kuna hoteli humo humo (bafeti, kama alivyotamka mama mmoja) lakini sikupata bahati ya kwenda huko. Pia kuna wakati walipita watu wengine watatu wenye sare, mmoja akiwa ni askari, walikuwa wanakagua tikiti (tiketi / ticket), walipofika kwangu nilimpatia kisha akaiminya na kidude fulani hivi cha rangi ya silva na kuweka alama ya 'V' kwenye tikiti hiyo.

Baadaye nikajipenyeza katikati ya miguu ya abiria waliokaa na kufikia dirishani, nilichungulia na kuona mandhari ya mapori vya vichaka vifupi, treni ilipofika kwenye kona nikaweza kuyaona mabehewa karibuni yote vizuri zaidi.

Kwa saa zaidi ya sita safari iliendelea...
*********

Hatimaye tuliwasili Tabora, nilishuka na kuelekea sehemu ya abiria kupumzika, nilishangaa kuwaona watu wengi wenye ugonjwa wa akili, wajasiri amali (siyo wajasiliamali) nao walichangamkia fursa ya kuwauzia abiria bidhaa zao...

Mara nikasikia tangazo lililonihusu kutoka kwenye kipaza sauti...

Nilifuatwa na watu wawili wa Kanisa la Morovian (MCWT), nikapelekwa hostel...

Kesho yake nikapelekwa Sikonge chini ya uangalizi wa MCWT na kuendelea na masomo huko hadi mwisho wa mwaka.

Nusu muhula nilibaki Mission ya MCWT Sikonge...

Disemba mwanzoni nirudi Kijijini Iramba, safari hii nilipewa 'Warrant' (karatasi fulani hivi ya 'light blue') ambayo ilikuwa kama tikiti safarini...

=

Kufika Kijijini, familia yangu ilifurahi, yule Padri Petro aliondoka kurudi kwao Latin America, alikuwepo Padri mwingine ambaye hakupenda jinsi nilivyopelekwa 'Morovian...' badala ya 'Roman...' (Nahisi walikuwa na mpango fulani ambao sikuujuwa). Hivyo sikupata ushirikiano mzuri kutoka misheni ya chemchem tena.

Mradi wa miti pale Misheni Chemchem ulisimama, baba alianzisha kitalu jirani na mto fulani hivi mbali kidogo na Mission ya Chemchem.

Nilitumia lori fulani hivi (Leyland Albion) maarufu kama "Kaza moyo" kwenda Singida kutokea kijijini, ama mabasi ya mzee Amri Said (Blue line baadaye Yellow line), kutoka Singida hadi Itigi usafiri ulikuwa wa mabasi ya 'Relwe.'

=

Niliendelea na masomo hadi nikahitimu darasa la nane 1967...

=

Mwaka huo kabla ya kuhitimu darsa la nane babu yangu mzee Bourne alifariki, aliugua ugonjwa wa kushindwa kuhema vizuri, alikuwa mtumiaji mzuri wa "goso / gozo" (tumbaku kali inayosokotwa kama sigara)

=

Mwaka 1969 nilichaguliwa kwenda darasa la tisa (form one) shule ya sekondari Tabora. (Tabora Central School, kama ilivyojulikana wakati inaanzishwa), nilijifunza mengi hapo ikiwemo mafunzo ya awali ya kijeshi. Nilihitimu mwaka 1972.

Mwaka 1975 nilihitimu kidato cha sita shule ya sekondari Kibaha. Mwaka uliofuata nilipata kazi ya muda National Milling Corporation (NMC) na mwaka mmoja baadaye nilipata ajira ya kudumu RTC (Regional Trading Company) Dar.

=

Wakati huo wote, sikuwa uhusiano wa kimapenzi 'serious', bali mabinti wa kijijini Iramba kwa kujificha sana.

Malezi ya ki-mission, huenda yalisababisha pia. Siku moja moja sana wakati nipo Kibaha nilikuwa napotelea Mwanalugali ama maili moja kupooza nye*ge.


Baada ya kuanza kazi NMC na kisha RTC ndipo 'ukiwembe' ulipoanza. Hata sijui nilipatwa na pepo gani!
**********

Nawaza historia ya maisha yangu, nikipotoka na hadi nilipo sasa, 'fujo' zote nilizofanya kuhusiana na uhusiano na mabinti mbalimbali...

"Naona sasa inatosha..." Nilijikuta nasema kwa sauti...

...Bado nilikuwa pale Shibam kijiwe cha keram. Jioni nilienda DDC kariakoo kwenye dansi, lakini wala sikuwa na 'mzuka' wala 'sikuopoa goma' (sikutafuta binti wa kustarehe naye)

Nilitumia siku ya jumapili jioni kumtembelea mzee Katibu Kata, alikuwa akiishi somewhere "kwa Ali Maua" Mwananyamala Dsm. Madhumuni yalikuwa pamoja na kumjulia hali, lakini pia kupata ushauri wake katika mawazo yaliyonijaa kuhusiana na Hamida, mtoto wa Mzee Burhani.


Nilikaa kwa mzee Katibu Kata hadi saa tatu usiku, hakuwa katika afya nzuri, malaria ilikuwa inamsumbua na alikuwa amemeza klorokwin (Chloroquine), dawa chungu kama muarobaini lakini pia zilikuwa zinamuwasha...

Tuliongea mambo mengi, lakini suala langu la kumchumbia Hamida lilichukuwa nafasi kubwa.

Aliniambia kuwa siwezi kufanikiwa kumpata binti Burhani, na sababu zake niliona zina mashiko. Kwamba, kwanza mimi ni mkristo, siwezi kufunga ndoa na binti Burhani ambaye baba yake ni mtu wa msimamo katika dini yake. Pia aliniambia kuwa Waarabu wana utaratibu wa kuoana wao kwa wao kama ilivyo kwa Wahindi. Ni nadra sana kukuta ndoa iliyo tofauti na hivyo, aliniambia.

Pia alinishauri kama kweli nimedhamiria basi kwanza kabisa nianze kumteka kimapenzi Hamida; Hamida ambaye hata hajui kwamba James 'amemzimikia'

Yaani nijitahidi nipate nafasi ya kuongea naye ili ajue nia yangu, nijue kama atanikubali ama la. Kisha ndio nianze mashambulizi kupitia Mshenga. Lakini pia alinishauri nijiweke sawa kisaikolojia na kuanza kufikiria kubadili dini.

Nilirudi home nikiwa na ahueni ya fikra, nilala vizuri usiku huo huku nikiwaza mambo mengi hususani pa kuanzia 'kumteka' Hamida kimapenzi.

Kwa wakati huo tayari nilikuwa mbobezi katika kufanya ngono na suala zima la mahaba, nikawaza sijui nitumie mbinu kama ya kwenye kitabu cha "Captive Bride"? Mwandishi Johanna Lindesy alisimulia kisa cha kusisimua sana katika kitabu hicho na harakati za kumteka umpendaye kisha atakupenda baadaye...

Wakati huo tayari nilikuwa nimeshasoma vitabu vingi vya falsafa ya mapenzi nk, nilikuwa najuwa nama ya kummiliki nimpendaye ipasavyo, sikuwa na hofu juu ya namna ya kuonesha mahaba yangu kwa Hamida, bali hofu ilikuwa namna ya kupata wasaa naye na kuanza kueleza 'neno la mapenzi'

Nilijimwagia maji (kuoga) na kulala huku nikiwa na ahueni.
*******

Kulipokucha kama kawaida ya siku za kazi huwa nawahi kazini kwa ajili ya kulisukuma gurudumu la maendeleo...

Nilifanya kazi nikiwa mwenye furaha sana kuliko mwanzo wa mwisho wa juma lililopita.

Baada ya kutoka kazini nilienda moja kwa moja hadi Magomeni Mwembe chai ambapo kulikuwa na kinyozi mzuri chini ya mwembe. (Alikuwa anatumia mikasi misafi, vitambaa vyake ni visafi na pia ananijulia kuninyoa)

Wakati huo nilikuwa nafuga nywele nyingi (afro / mchicha), hivyo nilienda kuziweka vizuri.

Baada ya kutoka hapo nilienda nyumbani kuoga na kubadili mavazi, chini nilivaa raba mtoni (raba toka Ulaya), nikavaa jeans ya bluu iliyokolea ya Levi Straus 501, mkanda mweusi wenye backle kubwa, nikavaa shati langu la picha ya ndege (a.k.a. Juliana), ndani nilikuwa nimetanguliza vest ya matobo matobo madogo (ilikiwa fasheni), mkonono nikavaa saa yangu Motima, nywele zangu afro nikazichana baada ya kuzipaka mafuta safi (hairtonic) Nilijipulizia pafyumu pendwa 'YU for Men', kisha nikatoka kuelekea Magomeni mapipa, pale yanapogeuzia Ikarus kwa pembeni kulikuwa na studio ya kupigia picha iitwayo Africa Studio.

Nilipiga picha tatu matata sana, moja nikiwa nimekaa kwenye kiti, nyingine nimesimama pembeni ya stuli ndefu ya studio na ya mwisho ilikuwa ni passport size. "Kwa hizi picha, Hamida hachomoi", niliwaza.

Wakati huo ilibidi kusubiri picha kwa siku nne ama tano hivi ili ziwe tayari. Hivyo sikukaa sana pale nikaelekea Shibam kwenye kijiwe cha Keram.

Niliwakuta watu wengi kama kawaida, niliwasalimia (vizuri safari hii), nikakaribishwa, kawaida yangu nikifika pale lazima niwapige round moja kwanza huku burudani zinaendelea...

Walikuwa wananipenda sana kwa hilo lakini pia kwa nafasi yangu RTC.

Wakati burudani, mabishano / mijadala inaendelea, nikaenda jirani na mzee Burhan (alikuwa hakosi hapo kila baada ya swala ya alasir) na kuanza kumdodosa...

" Mzee, nimeyafikiria maneno yako ya siku ile nimeona leo nije unipe muongozo" nilimuambia.

"Maneno gani tena?" Aliuliza.

Nikamkumbusha jinsi nilivyokosea kusalimia na kusema "salama leko" badala ya assalaam aleikum"

Akasemaa "ahaaaaa", kisha akacheka...

"Sasa mzee nafanyaje ili niwe mwislamu?" Nilimuuliza.

"Hebu twende nyumbani tukaongee vizuri" alisema huku akiwa amefurahi na kuanza kuinuka"

Moyoni nikasema "yes!, mwanzo huoo!

Kwakuwa hapakuwa mbali na hapo, batavuz yangu niliiacha nimeifunga vizuri, tukaanza kuelekea kwa nyumbani kwa mzee Burhan taratiib huku tukiongea mawili matatu.

Tukiwa njiani alinifundisha maana ya assalaam aleikum. Akaniambia kuwa maana yake ni 'amani iwe nanyi', na wa aleikum salaam maana yake ni ' nanyi iwe kwenu' yani hiyo amani. Nilifurahi sana kufahamu maana ya salamu hiyo na majibu yake.

Nikamwambia kuwa sisi waroma tunasalimiana 'tumsifu Yesu kristu' na tunajibu kwa kusema milele amina. Akaniambia kuwa anajuwa kwa kuwa kuna wakati aliwahi kwenda pale Moroco Hotel, Kanisani na kuwasikia waumini wakisalimiana hivyo mara kwa mara.

Tukafika kwake, akausukuma mlango kwa ndani bila hodi, ila akaniambia karibu sana kijana. Nikasema starehe.

"Karibu varandani" alisema huku akivua sandles zake na kutambuka (kuruka) kizingiti kuingia sebuleni.

Nami nikavua raba zangu kisha nikaingia. Mle ndani tuliwakuta watu watano wakiongea, alikuwepo yule mama Mwarabu, mama wa kiafrika, kijana wa makamo wa kiarabu, kijana mwingine wa kiafrika na mtoto mdogo (wa umri wa miaka mitano hivi)

Mzee Burhan alianza...

"Karibu sana James, huyu hapa ni mke wangu, maarufu kama mama Warda, yule pale ni mdogo wake (nilikuja kujuwa baadaye kuwa alikuwa msaidizi wa kazi aliyeishinao kwa miaka mingi sana), yule pale ni mwanangu anaitwa Yasir na rafiki yake..."

"Anaitwa Abdul" alidakia Yasir.

"Nashukuru kuwafahamu" nilijibu

"Eeee na huyu anaitwa James..." Mzee Burhani alimalizia akinioneshea mimi kidole....

"Tunamfahamu" walijibu wale vijana (Yasir na Abdul) kwa pamoja.

"Samahani, naomba mtupishe tuna maongezi nyeti kidogo" alisema mzee Burahani.
Yasir na Abdul walitoka nje kabisa ya nyumba, mama Warda na mdogo wake wakaenda chumba kingine...

Mzee akachukuwa Radio cassete recorder (Memory Q), akasogeza nilipokaa akaweka juu ya stuli kisha akaniambia kuwa atarikodi mazungumzo yetu ili awe na ushahidi...

"Hamidaaa" aliita yule mzee Burhani

"Abee baba" nilisikia sauti hafifu kisha nikasikia mlango unafunguliwa na hatua za kivivu zikawa zinasikika kuja upande wa sebuleni.

"Abee baba" alirudia kuitikia, safari hii sauti ilikuwa kama ile ya siku ya kwanza kumuona.

"Katuletee soda" Mzee Burhani alimuambia...

Kabla hajaondoka nikaijikuta nasema "Mie niletee togwa kama lipo"

Hamida hakusena neno, akaondoka...

"Huyu ni binti yangu wa mwisho, anaitwa hamida, ndio ametoka college juzi juzi, alikuwa akisomea mambo ya upishi." Aliendelea mzee Burhani.

"Nilikuwa watoto watano, Watatu wakike na wawili wakiume, dada yao mkubwa anaitwa Warda, kisha amefuatia Sabra halafu Yasir na Hamida ndio kitinda mimba. Mmoja alifariki. Huyo mtoto mdogo unayemuona ni mjukuu, mtoto wa binti yangu wa kwanza Warda" alinifahamisha.

Mara Hamida akaingia na chupa moja ya fanta na bilauli tatu.

Akaifungua ile soda na kumimina kwenye bilauli ndogo ambayo alimpa yule mtoto.

"Nadya, usimwage mwage eee!" Sauti nyororo ya Hamida ilisikika.

Kisha akamimina soda iliyobakia kwenye bilauli ya baba yake. "Karibu baba" alisema kisha akatoka tena.

Aliporudi alikuja na magi yenye togwa baridiii!, akasogeza redio pembeni kidogo, akachukua ile bilauli iliyosalia akaiweka kisha akamimina... " Karibu kaka" alisema na kuondoka.

Mie hapo moyo wangu burdani, nilikuwa nafurahia kila sekunde aliyokuwepo Hamida.

"Karibu James..." Mzee alisisitiza na kunitoa kwenye mawazo yaliyonijia ghafla.

"Enhe, umesema unataka muongozo kuhusu kubadili dini!" Alisema huku akibofya kitufe cha kuchezea kaseti sanjari na kitufe chekundu cha kurekodia.

"Ndio mzee, nipe muongozo" nilijibu baada ya kugida (kunywa) fundo (puff) moja ya togwa.

Akasema, sasa nitakuhoji maswali ambayo utakavyojibu itanipa mwelekeo...

"Je umelazimishwa ama kushawishiwa na mtu kubadili dini na kuwa mwislamu?" aliuliza

"Hapana mzee" nilijibu.

"Je huogopi kutengwa na jamii yako wakigundua kuwa umewahama?" Aliendelea kuuliza...

Niliinua bilauli ya togwa na kunywa tena, kisha nikamjibu, hapana, nimeshafikisha umri wa kuamua nitakalo, hivyo sina hofu yoyote.

Mzee Burhani akaniangalia kwa makini kisha akaniuliza kama najuwa uwepo wa mtu aliyeitwa Muhammad (s.a.w), nikamjibu, ndiyo nasikia alikiwepo mtu huyo.

Mzee aliendelea kunihoji imani yangu kuhusu Mungu. Nikamjibu "Sisi tunaamini Mungu ni mmoja na yupo katika nafsi tatu, yani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho mtakatifu"

Akaniambia wao waislamu wanaamini kwamba Mungu ni mmoja tu na hakuna Mungu mwana wala Mungu Roho mtakatifu...

Kwa kuwa nilishayavulia maji ilibidi nikubaliane naye katika kila alilozungumza, nilikuwa naona kama ananichelewesha...

"Sasa ili uwe mwislamu inabidi ukiri kwa moyo na kutamka kwa ulimi kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah na Muhammad ni mjumbe wake" alisema.

Aliniambia mengi ya awali kuhusu imani ya kiislamu ikiwemo kutosulubiwa kwa Yesu ambapo wao wanamuita Nabii Issa na mambo mengine kadha wa kadha.

Nikapata ugumu wa kiimani, kwani kusulubiwa kwa Yesu ndiyo msingi wa imani yetu ilipolala, lakini nikapiga moyo konde.

Akaniambia, nikajifikirie, kama nitakuwa tayari basi nimtafute ili anisilimishe rasmi na kunipeleka msikitini kwa ajili ya utambulisho.

Nikamjibu, sawa. Kisha nikamalizia togwa iliyobakia kwenye bilauli.

Alisisitiza kuwa kuwa muislamu ni rahisi sana, unatamka shahada mbili basi tayari unakuwa mwislamu.

Kwa kuwa jua lilizama tukiwa bado tunaongea, akaniambia anaenda kuswali (ndani) hivyo nimsubiri, kisha akatoka mle sebuleni.

Mara sauti za miguu ikitembea nikasikia ikija upande wa sebuleni.

Waooo! Hamida huyo! Nikijisemea kimoyomoyo, akakusanya zile bilauli na magi iliyobakia togwa shinda (kiasi) na kutaka kuondoka...

"Angalia usiangushe bilauli kama siku ile..." Maneno yalinitoka mdomoni...

Akatabasamu kisha akasema "hizi chafu hazitoanguka kwakuwa nimezibebanisha... Halafu siku ile ule mtandio ulikuwa unateleza sana..." Alijibu huku akimfuta Nadya alipojimwagia soda.

"Pole" nilimwambia kisha nikamuuliza "Eti malai (icecream) zipo?"

Akajibu kuwa zimebakia chache. Nikamwambia, nikitaka kuondoka naomba uniletee zote.

Akashangaa na kuuliza "sasa utazibebaje?"

Niwekee kwenye chombo kesho nitakuletea, naenda kuzihamishia kwenye chombo kingine ili niziponde ponde nitengeneze juisi.

Akacheka kisha akasema "si bora ungesema tu tukutengenezee juisi"

"Ewaaaaa (aiwaa) hilo pia ni wazo zuri, lakini leo nifungie, halafu naomba unitengenezee juisi nzuri ili nikinywa niwe nakukumbuka muangusha bilauli" nikasema.

"Mmh" akaguna na kuondoka.

Baada kama ya dakika kumi hivi nikamsikia mzee Burhani akikohoa huku akija uelekeo wa sebuleni.

"Samahani nilikuacha peke yako" alisema huku akiingia.

"Bila samahani, sikuwa peke yangu, Hamida alikuwepo na huyu Nadya pia..." Nilisema huku nikikaa vizuri kwenye kochi.

Hatukuongea sana baada ya pale, nikaaga na kutaka kuondoka, nikamuambia nimeagiza niletewe malai...

"Hamidaaaa" Mzee Burhani aliita.

"Mgeni anataka kuondoka"

Mara akaja na kiboksi kidogo cha kuhifadhi joto (ama baridi), akanipatia.

"Shilingi ngapi?" Nikamuuliza kwa sauti ya chini.

"Shilingi nne, zipo nane humo" alijibu.

Nikatoa gwala (dala/ shilingi tano) nikampatia, nikamwambia chenji nitachukuwa kesho.

Akasema "in shaa Allah."

Tukasimama na mzee Burhani kwa pamoja, nikachukuwa kiboksi chenye malai na kutoka sebuleni, nikavaa ndaba (raba mtoni) zangu na mzee Burhani akanifungulia mlango, akanisindikiza hadi Shibam (siyo mbali), nikamwacha hapo, nikachukuwa batavuz yangu huyoo hadi Butiama restaurant kisha nyumbani.
*******

Nilikuwa na furaha kubwa sana, kupata wasaa wa kuongea na mzee Burhani na kubadilishana maneno na Hamida.

Ghafla tafakari za imani ya dini yangu ikanijia, nikaanza kuwaza mabadiliko yatakayojitokeza kama nikisilimu.

Kupoteza mawazo nikachukuwa zile icecream na kuzipondaponda kisha nikaweka kwenye friji. Nikachukuwa sehemu ya ile juisi(vibarafu vidogo vidogo) na kuweka kwenye glasi kisha nikachukuwa brandy kabatini na kumiminia kwa wingi hadi glasi ikajaa.

Kiukweli wala sikuwa nahitaji icecream, nilitaka tu nipate wasaa wa kubadilishana maneno ya Hamida, "nimefanikiwa hivyo ngoja nishangilie ushindi wa awali." Nikijisemea kisha nikaanza kunywa taratiibu huku nikisikiliza santuri ya Kool and the Gang, wimbo wa 'Celebration'
************


Alarm ya saa ya mezani iliniamsha saa kumi na mbili asubuhi, ndio nikajuwa kuwa nilikunywa kupita kiasi, turntable ilijizima yenyewe (changer), taa sikuzima, na nilishtuka nikiwa sebuleni kwenye kochi.

Kumbe niligigida mzinga wote wa Cognac Brandy. Kichwa kilikuwa kizito, na ilikuwa Jumanne.

Niliamka kujiandaa kwenda kazini.

=

"Habari za asubuhi Marry?" Nilimsalimia mhudumu ofisini kwangu .

"Nzuri boss, karibu" alinijibu huku akipokea mkoba wangu mdogo.

"Leo najisikia vibaya kidogo, hivyo napumzika ofisini kwangu hadi saa nne, baada ya hapo utaruhusu watu kuonana nami" nilimwambia.

"Sawa boss" alijibu huku akiendelea na usafi.

Niliingia ofisini na kukaa kwenye dawati langu huku nimeinama.

"Karibu chai boss" Marry alinistua...

"Oh, ahsante, eeeeh hebu nenda pale mgahawani kaniletee supu maridadi" nilisema huku nikijiweka sawa.

Nikaiangalia ile chai, nikaona haipandi kabisa asubuhi ile. Hivyo nikaanza kupekua mafaili yangu wakati nikisubiri supu, huku nawaza mambo mawili makuu, kusilimu na kuanza kumtongoza Hamida.
******

Haikupita muda mrefu nikaletewa supu ya ng'ombe ya moto safi kabisa, nikainywa na kula nyama, nikaanza kujisikia ahueni.

Niliendelea kufanya kazi kivivu vivu huku nikiwaza mengi kichwani...

Niliwaza jinsi harusi za kwetu utaturuni zinavyokuwa, niliwaza jinsi wanawake wa kitaturu wanavyojuwa kuwanyenyekea wanaume, niliwaza kuhusu sherehe zinavyokuwa, niliwaza msisimko wa nyimbo na hamasa zenye kuamsha hisia kali... Ilimradi niliwaza mambo mengi kuhusiana na mambo ya harusi.

"Kweli sasa nimekua" nilijikuta nasema kwa sauti.

"Vipi boss, leo mbona uko hivyo? siyo kawaida yako!" Marry aliniuliza alipokuja kuchukuwa vyombo pamoja na kuleta mafaili mengine ya kuyapitia...

"Eeeeh, nafikiri muda wangu wa kuoa sasa umewadia" nilimjibu huku nikitabasamu

"Heheeee!" Alicheka kiumbea

"Vipi, huamini?" Nilimuuliza huku natabasamu

"Hapana, naamini ila najiuliza ni nani huyo aliyekukamata hadi umetangaza ndoa" alisema.

"Hapana, sijatangaza ndoa, wala mchumba mwenyewe hajui kama atatongozwa..." Nikasita kidogo kisha nikaendelea...

"Nataka nioe Mwarabu" nilimalizia.

"He!" Alishangaa na kuondoka.
**********

Marry ni mfanyakazi hodari sana, ni Katibu muhtasi wa siku nyingi (nilimkuta kazini) na anapenda sana utendaji wangu.

Huwa namshirikisha mambo yangu mengi, na huwa ananishauri vizuri.

=

Jioni baada ya kutoka kazini moja kwa moja nilielekea kwa Alimaua kumtembelea mzee Katibu Kata.

Nilimkuta ana nafuu sana kuliko juzi yake. Nikamweleza maamuzi niliyofanya ya kuanza kubadili dini na kisha muanza kumpa maneno ya mapenzi mchumba mtarajiwa.

Alifurahia uamuzi wangu wa kuamua kuingia katika 'dini yake', lakini hakuwa na matumaini kama nitafanikiwa kumuoa Hamida kwa jinsi alivyokuwa anazifahamu familia za Kiarabu.
*****

Mzee Burhani ana asili ya Oman, Babu yake alikuja miaka mingi kabla ya uhuru, alikuwa anaishi kisiwani Unguja. Baba yake mzee Burhan marehemu alhaj Ahmed Said alihamia Dar es Salaam katika harakati za kibiashara na yeye mzee Burhani alizaliwa hapo Dar.

Mke wake ni half-cast wa kingazija na kihindi, yaani baba yake alikuwa mgazija na mama yake alikuwa ana asili ya kihindi waliolowea Comoro.

Mchangachiko huo ulitoa matunda mazuri ya watoto wa kike ambaye kitinda mimba wao ndio nafikiria jinsi ya kumuingia na kumtongoza.

Kaka yake Hamida aitwaye Yasir pamoja na rafikiye Abdul wote ni madereva wanaendesha malori (Scania 81). Wiki hiyo magari yao yalikuwa Kibaha (Sub-Scania) kwa ajili ya service kubwa, ndiyo maana walikuwa wanaonekana mjini muda mwingi.

Warda ameolewa na mtoto wa baba yake mdogo, yupo Mwanza, Sabra ameolewa pia na ndugu yao wapo Oman, Yasir bado hajaoa.
********

ITAENDELEA

No comments