Breaking News

UHUSIANO WANGU KIMAPENZI NA HAMIDA - 2



Simulizi : Uhusiano Wangu Kimapenzi Na Hamida
Sehemu Ya Pili (2)


Tuliongea mengi na mzee Katibu Kata, akanitia moyo japo alikuwa anahisi 'nitagonga mwamba' katika harakati zangu za kumchumbia Hamida.

Nilivyotoka Mwananyamala moja kwa moja nilielekea nyumbani, baada ya kupumzika nilielekea Butiama Restaurant, tayari ilikuwa jioni, nilienda kwa mzee Burahan kurudisha 'coolbox' yao, na kuchukuwa juisi nzuri ya mikomamanga iliyochanganywa na embe ng'ong'o.

Aliyenipokea alikuwa Yasir, kaka yake Hamida, alipokea lile boksi kisha akamwita Hamida apeleke jikoni.

Hamida alivyokuja alinikuta bado nimesimama ukumbini (koridoni)...

"Huingii varandani leo" Hamida aliuliza huku anakuja

"Hapana, leo nina haraka..." Kabla sijaendelea alinikatisha...

"Basi subiri nikuletee juisi" alisema.

"Sawa" nilimjibu.

Punde si punde alirejea dumu la lita 3 lililojaa juisi. Nilipokea na kumlipa, nilijifanya sina stori siku hiyo, nikaaga Nilielekea home.
*******

=

Siku tatu baadaye jioni nilipotoka kazini, ilikuwa siku ijumaa, nilitoka mapema kuliko kawaida yangu...

"Naenda kwenye mawindo ya binti mwarabu" nilisema baada ya kumuaga Marry.

"Haya boss, usinisahau kwenye kamati ya maandalizi..." Alijibu kuhu akitabasamu.

Nikaenda nyumbani moja kwa moja, nikaoga na kubadili nguo, (nilivaa 'bora shoes', suruali ya kitambaa, tshirt nyeupe) nikatoka nikaenda moja kwa moja hadi Africa Studio, nikakuta picha zipo tayari (black & white), zilikuwa zimetoka vizuri mno. Wakaziweka kwenye bahasha (B5) nyeupe, nikamalizia malipo nikaelekea Shibam.

Pale Shibam sikumkuta mzee Burhani, niliwapiga round moja ya kahawa kisha nikaelekea nyumbani kwa mzee Burhani.

Nilikaribishwa vizuri na yule mama wa kiafrika na kuingia sebuleni. Sebule yote nikaibadilisha harufu na kuanza kunukia uturi (perfume) ya Gift of Zanzibar. Ilikuwa inanukia vizuri sana, kama udi hivi lakini siyo, kama asmini hivi lakini siyo, ilimradi ni harufu isiyochosha wala kukera.

Baada ya kusalimiana, nikamkabidhi lile dumu la juisi, halafu nikamwambia kuwa nina shida na mzee.

Akanijibu mzee yupo chumbani kwa Hamida wana mazungumzo na wanawe.

"Kuna posa (ya maneno) imeletwa ndio wanajadili mzee, mama Warda, Hamida na Yasir." Alisema.

Ghafla moyo ukaanza kunidunda kwa nguvu, nadhani hata yule mama aligundua.

"Sawa mama, nasubiri wakimaliza watanikuta" nikamjibu.

"Basi ngoja nikuletee kinywaji chako ukipendacho" alisema huku akiinuka

"Sawa mama" nilijibu.

Aliniletea bilauli iliyojaa togwa baridi, akavuta stuli na kuniwekea.

"Karibu" alinikaribisha.

"Ahsante mama" nilisema kisha nikaweka bahasha yangu kwenye stuli.

Nikaanza kunywa mdogo mdogo huku nikiwa na mawazo.

Akatoa ukimya kwa kuniuliza, imekiwaje nalipenda togwa, nilimjibu nilijifunzia kunywa Iramba ambako ni kinywaji cha kawaida.

Akahoji "wewe nyiramba"
Nikamjibu "hapana"

"Mnyaturu?"
"Hapana"

"Ishi, sasa wewe ni kabila gani?" Aliuliza.

"Mimi ni Mtaturu" nilimjibu

"Ahaaaa, nyie ndio Mang'ati eee" alisema kwa kutania

"Hapana, ila tunashabihiana sana, wote asili yetu ni Ethiopia, lakini mababu zetu walihamia miaka mingi sana maeneo ya Arusha - Manyara (wakati huo Manyara ilikuwa sehemu ya Arusha)

" Ahaaa, ndio mkaanza kuwaibia wamasai ng'ombe zao eeee!" Alitania

Nikacheka kisha nimasema "Hapana, sisi ndiyo tulikuja na mifugo kutoka Ethiopia, babu zetu walikuwa wakibadilishana mifugo na wenyeji kupata ruhusa ya kukaa sehemu kabla ya kufika ardhi waliyoipenda ambapo ni kandokando ya ziwa Eyas. Hivyo zote hizo ni ng'ombe zetu...." Nikacheka tena kisha nikaendelea, "Hata zile za Usukumani ni za kwetu pia" nilitania...

Nilikuwa nadhani yeye ni msukuma kwa lafudhi yake wakati anaongea.

"Unafikiri mie msukuma, mie ni Mnyamwezi" alisema na kucheka kiasi

Nami nikacheka. Hakika aliniondoa kwenye mawazo yaliyotaka kuniteka ghafla.

"Basi togwa hilo ni la Tabora" alisema,

"Mie ndio nimewafundisha humu ndani kulitengeneza, niko nao hawa tangia usichana wangu hadi sasa, kuna wakati niliondoka nikaolewa nikazaa watoto 7, lakini ndoa haikuwa ya furaha sana, nikaomba talaka, ndipo niliporudi hapa hadi sasa." Alisema huku akionesha huzuni kiasi.

"Du, pole sana", nilimwambia, na kumuuliza watoto wake wako wapi.

Alinijibu kuwa wote wapo Tabora kwa baba yao.

Mazungumzo yetu yalikatishwa pale Yasir alipoingia sebuleni, alisalimia na kuketi. Haikupita muda mama Warda naye akaingia, tukasalimiana, kisha akatania "umefuata ice cream na leo?", nikamwambia hapana, leo nina shida nyingine na mzee, mara mzee naye akaingia. Tukasalimiana kisha akasema "samahani, nimekusikia umekuja muda kidogo, lakini tulikuwa tuna mazungumzo ndani, binti yangu ameposwa, lakini hataki kuolewa ndiyo tulikuwa tunayajenga..."

Da! Kimoyomoyo nilifurahi sana, nikaona hii ni dalili njema kwangu, hofu na wasiwasi juu ya kumkosa Hamida ukaniondoka.

"Ahaa, haina neno, mie nilikuwa na mama huyu sikuwa mpweke" nilijibu.

"Naam, twaib, nakusikiliza, au ni faragha niwaombe hawa watuachie nafasi?" Mzee Burhani alisema.

"Hapana, siyo siri, nimekuja naomba unisilimishe, nimeshakata shauri" nilisema.

"Allahu akbar" alisema mzee Burhani.

"Hamidaaaa" mzee Burhani alimuita binti yake.

Mara Hamida akaingia, kimyakimya, macho mekundu, sura imemvimba kama alikuwa analia. Akaketi jirani na yule mama wa kiafrika.

Pakawa na ukimya fulani hivi wa sekunde chache, kisha mzee Burhani akakata ukimya kwa kusema...

".... Eeeh bila shaka nyote mnamfahamu James, wiki iliyopita tulikuwa hapa tunazungumza, alikuja kuomba muongozo akitaka kusilimu. Nilimpa mawili matatu na leo amekata shauri na kutaka kusilimu."

Alitulia kidogo kisha akaendelea...

"Binadamu wote kwa asili tunazaliwa waislamu, lakini wazazi wetu ndio hutubadili dini na kufuata dini nyingine ama kubaki katika dini ya asili ambayo ni uislamu..."

Aliendelea na hotuba isiyo rasmi...

"Uislamu ni Amani, kama lilivyo neno lenyewe, ni kujisalimisha kwa Mola Muumba wa mbingu na nchi na kunyenyekea kwake, hivyo basi umefanya uamuzi sahihi kurejea katika dini ya asili ambayo ina mfumo mzima wa maisha ya mwanadamu wa namna ya kuyaendea mambo yake hapa duniani, kaburini, siku ya ufufuo na hukumu na baada ya hukumu." Alisimama kidogo kumeza mate kisha akaendelea...

"Shahada mbili ni mkusanyiko wa matamko mawili ya ahadi anayoichukua kiumbe (mwanadamu) mbele ya Muumba wake na viumbe wenzake; mbapo mtamkaji hula kiapo cha utii kwa Mwenyezi Mungu (Allah) na Mtume wake katika maisha yake yote kwa kufuata maamrisho na makatazo yake."

"Shahada ya kwanza ni tamko la utii kwa Allah, na shahada ya pili ni tamko la utii wa mtume wa Allah..."

"Sasa nitasema maneno nawe utafuatisha..."

Nikaitikia sawa.

"Nitaanza kusema kwa kiarabu kisha tutarudia kwa kiswahili ili uelewe maana yake" alisema, kisha akaanza kutamka...

Wakati huo wote sebuleni palikuwa kimya, nami namsikiliza mzee Burhani kwa makini huku nikiibia kumuangalia Hamida, alikuwa amejitanda uso wote kwa mtandio kasoro macho tu ambayo yalionekana kuwa mekundu kuliko kawaida.


“ASH-HADU"
Nikafuatisha,
(Ash-hadu)

"AN LAA"
(An-laa)

"ILAAHA"
(Ilaaha)

"ILLAL-LAAHU”
(Illal-laahu)

“WA ASH-HADU"
(Wa ash-hadu)

"ANNA MUHAMMADAN"
(Anna Muhammadan)

"RASUULU LLAH”
(Rasuulu llah)

"NASHUHUDIA KWA MOYO NA KUTAMKA KWA ULIMI KWAMBA"

Nikaendelea kufuatisha...
(Nashuhudiabkwa moyo na kutamka kwa ulimi kwamba)

"HAKUNA MOLA APASWAYE KUABUDIWA KWA HAKI ISIPOKUWA ALLA"
(Hakuna Mola apaswaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah)

"PIA NASHUHUDIA KWA MOYO NA KUTAMKA KWA ULIMI KWAMBA"
(Pia nashuhudia kwa moyo na kutamka kwa ulimi kwamba"

"MUHAMMADI NI MJUMBE WA ALLAH"
(Muhammad ni mjumbe wa Allah)

"kama alivyo Yesu, Mussa, Ibrahimu" alimalizia kisha wote mle ndani wakasikika wakisema, Allahu akbaru, Allahu akbaru, Mungu ni Mkubwa, Mungu ni Mkubwa.

Walisema maneno hayo (Allahu akbaru) hata kabla sijayafuatisha maneno ya mwisho ya mzee Burhani.

Kisha nikamuona Hamida, Yasir na mama Warda wanalia kwa kutokwa na machozi bila kutoa sauti...

Pakawa na ukimya kidogo...

Nikawa nawaza, hivi hawa wanaolia, wanalia kwa sababu nimesilimu ama kuna jambo jingine!

Nilikuja kujuwa baadaye sana wakati mtu mwingine aliposilimu nikishuhudia, kuna hali fulani ya utii na unyenyekevu wa imani (emotions) hujaa...

"Sasa James umeshakuwa mwislamu, inabidi uchague jina zuri ulipendalo ili uitwe kwa jina hilo" mzee Burhani alitoa ukimya uliokiwepo.

Tayari kichwani nilikuwa nina jina nililolipenda ambalo lilianzia na herifi J kama jina langu.

"Jamaal" nilitamka

"Maa shaa Allah, Jamaal maana yake ni mzuri, wa kupendeza yaani handsome..." Alidakia mzee Burhani.

"Kuanzia sasa tutakuwa tunakuita Jamaal" aliendelea...

"Sasa kuna mambo muhimu ambayo unapaswa kujifunza ili uyajuwe ukishakuwa mwislamu, nitakupatia vitabu ili uweze kujisomea mambo muhimu, yameandikwa kwa kiswahili pia vipo vitabu vya kwa lugha ya kiingereza..." Aliendelea

"Kwakiwa wewe ni mtu mzima, inabidi upate mafunzo ya dini kwa njia tofauti siyo kama watoto wanavyofundishwa, chaguwa siku za kujifunza nami nitakutafutia mwalimu"

Nikamjibu

"Mie nipo tayari siku nne kwa wiki, yaani Jumatatu hadi Alhamis baada ya kutoka kazini nakuwa huru, hivyo nakusikiliza wewe mzee"

"Yasir hebu kalete kile kitabu cha swala na mafundisho / maamrisho yake" mzee Burhani alimwambia kaka yake Hamida

"Naona muda wa swala umewadia, sasa twende wote msikitini" alisema mzee Burhani huku akiwa mwenye furaha.

Mie sikuwa na hofu wala kipingamizi, nilishayavulia nguo maji inabidi niyaoge.

Yasir alirudi na kitabu kidogo kiitwacho Sala na maamrisho yake na kunipatia.

Kwakuwa kilikuwa kidogo sana, nilikiingiza mfukoni mwa suruali.

Mzee Burhani akasimama, nami nikasimama tukatoka tukawa tunaelekea msikitini. Tulielekea msikiti wa Mkauni, siyo mbali kutoka kwa mzee Burhani.

Nyuma yetu Yasir alitufuata, tukawa tunaambatana naye, tulivyofika msikitini, tukavua viatu kama kawaida, tukavi hifadhi sehemu ya kuhifadhia, kisha mzee Burhani akamwambia Yasir anifunidhe namna ya kuchukuwa udhu ili niwe tayari kwa ibada ya swala.

Yasir alinielekeza msalani, baada ya kutoka msalani akanipeleka sehemu maalum ya kutawadhia (kuchukuwa udhu), yaani kuosha viganja vya mikono, kusukutua, kusafisha pua, uso, mikono yenyewe hadi viwikoni, kupaka maji kwenye kichwa na masikio kisha kumalizia na kuosha miguu.

Nilifanya kwa kumuigiza afanyavyo, tulipokuwa tayari tuliingia ndani tayari kwa ibada...

Baada ya kuswali (inachukuwa dakika tano hivi) nikasikia tangazo...

"Kuna kijana amesilimu, alikuwa akiitwa James Jasson na sasa ataitwa Jamaal Jason, alikuwa dhehebu la Roman Catholic, tunamuomba asimame ili waislamu tumuone tumjue kuwa ni ndugu yetu katika imani"

Ni imamu (kiongozi wa ibada) alikuwa akitangaza.

Wakati nainuka nilisikia Allahu akaru nyingi hadi nilisisimkwa mwili, nikaombewa dua, kishwa waumini wakaambia wawe wananisaidia katika mambo ya ibada na kadha wa kadha.

Baada ya tasbihi (kama kusoma rozali vile) na dua, watu walianza kutoka, mzee Burhani alikuwa anaongea na Imamu, bila shaka ndiye aliyempa taarifa za kusilimu kwangu.

Kisha nikaona mzee Burhani amesimama tena peke yake akawa anaswali.

Mie na Yasir tukatoka nje tukawa tunamsubiri.

"Eti, mbona nilimuona Hamida akilia, kulikoni" niliuliza kiuchokozi

"Aaaa ni stori ndefu nitakuhadithia kesho in shaa Allah" alijibu kifupi namna hiyo, na mara mzee Burhani akawa anatoka nje.

Tulirudi wote hadi nyumbani kwa mzee Burhani, lakini sikuingia ndani, bali niliagana nao nikapanda batavuz yangu huyooo hadi Butiama restaurant, kisha nyumbani.
**********

Nilivyofika nyumbani nilikipitia kile kitabu na kuona yaliyoandikwa, ni kitabu kidogo sana unachoweza kusoma kwa saa chache tu.

Nilikuta misamiati mingi ambayo sikujuwa maana yake mara moja, lakini kilikuwa kinaeleweka vizuri tu.

Baada ya kujimwagia maji na kujifuta, nikajilaza kitandani chalichali nikiwa nimevaa bukta huku nikitafakari safari ambayo nimeianza.

Nikawa nawaza, hapa pombe tena basi, kuzini tena basi nk hadi nikapitiwa na usingizi.
********

Sikwenda sinema ijumaa hiyo kama ilivyo kawaida yangu. Kesho yake mapema sana nikaenda kwa mzee Katibu Kata, niliwahi ili asije kuondoka nyumbani kabla.

Nilimueleza habari yote ya kusilimu kwangu, akafurahi sana, tukabadilishana maneno mawili matatu kisha nikamuaga huyooo hadi nyumbani.

Niliendelea na shughuli ya usafi hadi niliposikia adhana, nikaacha, nikajitayarisha kwenda msikitini. Kutoka nyumbani hadi msikiti wa mkauni ni mbali kidogo kwa kutembea kwa miguu, hivyo niliwasha batavuz nikaenda.

Nikifuata utaratibu kama wa jana usiku hadi ibada ilipoisha nikatoka na kuelekea Butiama. Hakika Butiama Restaurant nimewachangia sana!

Baada ya hapo nilirudi nyumbani kumalizia usafi na mambo mengine.
****

Saa kumi baada ya swala ya alasiri nilienda Shibamu, siku za Jumamosi watu huwa wengi wakijiburudisha kwa michezo mbalimbali.

Mara mzee Burhani akawasili...

"Ahaaaa sheikh Jamaal, upo?" Alisema baada ya kusalimia watu waliokuwepo pale...

"Jamani eee, kuanzia jana huyu James sasa tumuite Jamaal, amesilimu." Alisema

Allahu akbaru, watu waliokiwepo pale walisema maneno hayo kwa kurudia mara tatu.

"Karibu sana Jamaal" mzee mmoja maarufu sana kijiweni hapo alisema.

Mzee Burhani akaniambia, mwalimu wako wa awali atakuwa mwanangu Yasir, wiki hizi mbili yupo tu anasubiri gari iwe tayari, iko service kubwa.

Sasa basi Jumatatu utaanza naye hadi atakapoondoka kisha nitakuwa nimeshapata mwalimu utakaye endana naye kukusomesha mambo muhimu.

Tuliongea palee hadi magharibi ilipofika, baada ya swala akanikaribisha kwake kwa chakula cha usiku.

"Umri wako unaruhusu kuoa, utakula hotelini mpaka lini" alitania

"Bado natafuta mke muafaka" nilijibu...

Tuliendelea na mazungumzo ya dini hadi ilipowadia muda wa swala ya isha. (Swala ya saa mbili usiku)

Baada ya kuswali, tulirudi nyumbani kwa ajili ya chakula cha usiku.
*****

Sebuleni kuliandaliwa chakula kizuri sana, kulikuwepo viazi mbatata (viazi mviringo), sijui hata wamevifanyaje, maana ni vilaini pia vina kama mbogamboga (nilijuwa baadaye kuwa ni kachori), mchuzi wa nyama ya ng'ombe pamoja na nyama yenyewe, chapati maridadi sana, sikuwahi kuziona kama hizo kabla, wali uliopikwa kwa nazi, mchuzi shatashata wa kamba / kaji (prowns), chai ya maziwa na ya mkandaa (black tea), kisamvu kilichokolea nazi.... Bila kusahau pembeni kulikuwa na jagi la maji ya kunywa.

Mtihani ukawa namna ya kukunja miguu wakati wa kula maana pameandaliwa kwenye busati juu yake paliwekwa mkeka.

Baada ya kujikunja vizuri nikifanikiwa kukaa ipasavyo, ni mkao unaoweza kukaa hivyo kwa muda mrefu bila kuchoka (miguu inakunjwa kwa kupishana kama unaikalia lakini huikalii)

Kwa kuwa sebule ilikuwa kubwa sana, kuliandaliwa sehemu mbili, jirani na pazia la mlango walikaa mama wa Kiafrika, Hamida, Nadya na mama Warda, na upande mwingine tulikuwa mimi, Yasir na mzee Burhani.

Mie nilikaa kwa namna ambayo nilikuwa naangakiana uso kwa uso na Hamida japo kuna ka-umbali hivi.

Nilishazoea kula kwa kijiko, leo najifunza kula kwa mikono, nilisema hivyo wakati Yasir akinimwagilia maji ya kunawa...

"Utaweza tu Jamaal" alijibu.

Sikutaka kuanza kula wali kwa kuwa nimeshauzoea, nilianza kula chapati kwa mchuzi na chai,  Hakika kuna watu wanajuwa kupika jamani... Nilijikuta nasema tu kwa sauti...

Nilivyomaliza chapati moja nikahamia kwenye kachori, dah, tamu sana, zina pilipili kwa mbaali, mwisho nikapakuwa 'tuwali' kiduchu ili nimalizie, loh salaleh, kumbe bwana ule wali ndio funga kazi, nikaongeza mwingine mwingi...

Mchuzi wake sasa na prouwns waliokaangwa na kumenywa kisha kuungwa kwa nazi nzito, acha kabisa..., utamu wa kisamvu sijawahi kula popote pale... (Kilitwangwa jana yake na kuchemshwa kwa viungo muafaka, leo ndio kimeungwa vizuri kwa nazi, hii aliniambia Hamida siku nyingine kabisa nilivyomuuliza)
*****

Baada ya kula, tukawa tunazungumza mambo ya kawaida, hali ya uchumi wa nchi, kupungua kwa bidhaa muhimu nk

Wakati huo Hamida alikuwa bize akiondosha vyombo...

Aliporudi alikuja na bahasha yangu niliyoishau jana (kwa makusudi)

"Jana ulisahau mzigo wako" Hamida alisema huku akinipatia bahasha ambayo tangia awali sikuwa nimeifunga kwa lengo maalum.

"Ooh, ahsante, nilishasahau kama zipo hapa" nilijibu

Lengo langu lilikuwa Hamida anione vizuri kwakuwa mara zote niwapo hapo huniangalia kwa kuibia ibia tu.
*******

Niliaga, Yasir akaniambia ngoja nikusindikize....

Nilikokota batavuz huku tukielekea maeneo ya Shabam kutokea nyumbani kwa akina Hamida...

Njiani wakati tunaongea mawili matatu ndipo nikachomekea kuhusu kulia kwa Hamida...

Akanieleza kuhusu posa iliyokuja kutoka Oman, na kwamba muoaji alikuwa mtu mzima sana lakini tajiri... Hamida alikuwa hataki kuolewa na mtu mzima hivyo walikuwa wanajaribu kumsihi akubali kwani ndiyo posa ya kwanza na umri wake ulikuwa umewadia kuolewa...

Hamida alimaliza kidato cha nne miaka miwili iliyopita kisha akaenda Kenya kusomea stashahada ya domestic science na catering (Kenya Utalii College - Campas ya Mombasa).

"Du" nilisema
"Lakini yafaa apewe uhuru wa kuchaguwa ampendaye, kama hamtaki msimlazimishe, asije akachukuwa maamuzi mabaya" nilisema

Kipindi hicho mabinti kuzaga chupa na kumeza kwa ajili ya kujiua ilikuwa tabia iliyoshamiri sana.

Tuliagana yeye akarudi na mie nikapanda batavuz yangu hadi home nikiwa na furaha sana kwa kupiga hatua nyingine kwenda 'mbele'.
*******

*******************

Siku ya Jumapili nilitulia nyumbani kwa ajili ya kunyoosha nguo na kujisomea.

Baadaye nilianza kufikiria jinsi ya kuanza kumtongoza Hamida.
******

Enzi hizo kupata mpenzi wa kudumu naye unasotea haswa, hasa katika mazingira magumu kama haya ya geti kali na msimamo wa kidini.

Kwakuwa tayari nimepata tiketi ya kuwa na Yasir siku nne kwa wiki japo kwa saa chache, niliona ni nafasi nzuri ya kutimiza azma yangu...

Siku ya Jumatatu niliwahi afisini kama kawaida yangu, niliingia huku napiga mluzi

"Karibu boss, habari za asubuhi? Marry alinisalimu wakati naingia afisini kwangu...

" Njema sana bibie, ukimaliza kazi zako uje afisini" nilimuambia.

Nilifanya kazi baadaye nikaletewa chai, nikamwambia Marry aketi niongee naye huku nakunywa chai...

"Zoezi la kumnasa mwarabu limeanza, Ijumaa nimesilimu" kikanyanyua kikombe nikanywa chai kidogo

"Enhe!" Alishabikia

"Ndiyo hivyo, sasa naitwa Jamaal, japo sinto badili kwenye makaratasi kiserikali, ila wewe tambua mimi ni Muislamu na jina langu ni Jamaal" niliendelea

"Huyo bibie kweli amekuweza, yani ulivyokuwa hushikiki leo umetulizwa, kweli hakuna mkate mgumu kwenye chai" aliongea huku akicheka.

Marry tunaelewana sana, wakati mwingine nilikuwa namshirikisha kufanikisha kupata warembo wa kustarehe nao, yaani kifupi nilikuwa kiwembe balaa!

Lakini tangia nimuone Hamida mara ya kwanza, nikawa kama pepo la uzinzi limenitoka vile, maana sikutamani tena wanawake. Nilikuwa namtaka yeye tu, hadi nimpate tena kwa kumuoa kabisa.

Tuliendelea kuongea na Marry hadi walipoingia wageni, mie nikaendelea na kazi zangu naye akawahudumia wageni (wateja)
****

Muda wa kutoka kazini ulipowadia nilienda nyumbani, nikabadili nguo kisha nikaelekea kwa mzee Burhani kwa mwalimu wangu Yasir.

Tulianza masomo ya Qur'an, alianza kunifundisha herufi za kiarabu, (abt... Aliif, bee tee..) Hadi mwisho na kuniambia nizidurusu hadi nizikariri hadi mpangilio wake. Alinifundisha herufi 30 japo aliniambia zipo zingine lakini kwa mpangilio wa kuzichanganya.

Aliporidhika ninazitamka vizuri, alitoka akaniacha na kuniambia niendelee kuzisoma zote kwa sauti (siyo ya juu bali ya kusikia) hadi atakaporudi.

Sehemu niliyokuwa nasomea ilikuwa chumba kinginge ambacho huwa wanakitumia kuswalia wanaoswalia nyumbani.

Chumba si kikubwa kama pale sebuleni, kuna zulia zuri la kijani, kuna miswala iliyokunjwa mitano, hakuna vitu vingine bali misahafu.

Kabla ya jua kuzama, nikaona mtu anaingia, kumbe Hamida, mkononi ameshika bilauli...

"Pumzika kidogo, nimekuletea togwa..." Alisema

Nikaacha kusoma, nikapokea na kumuuliza

"Na hili umelitengeneza wewe?!

"Hapana leo sijaliandaa mimi, ma-mkubwa ndiyo ameandaa" alijibu.

"Ahaa, basi kesho niandalie kinywaji utakachotengeneza wewe" nilimuambia

"Unafikiri mie sijui, ndiyo fani yangu ati" alisema kwa kulegeza ulimi ile lafudhi ya kimombasa

"Haya basi nione ufundi wako hiyo kesho" nilimjibu. Kisha akatoka.

Mara Yasir akaingia na adhana ya magharibi ikaanza.

"Twende zetu masjid" Yasir alisema

Bila kujibu kitu nikainuka, tukatoka nje na kuelekea msikitini.

Njiani aliniuliza kama nimehifadhi herufi zote, nikamwambia tukitoka msikitini nitamsomea ili ahakiki.

Baada ya ibada tulirudi kwao na kuingia chumba kile kile cha kusomea na akaanza kunisikiliza.

Kuna herufi chache nilikuwa nakosea kuzitamka ipasavyo, akanirekebisha kisha akaniambia ngoja akanunue daftari ili niziandike.

Kumbe wakati nasoma, walikuja akina Hamida, mama yake na mama mkubwa kwa nje (koridoni)/walikuwa wananisikiliza...

Hamida akaingia na kuniambia...

"Ma shaa Allah hodari kumbe, mara hii umehifadhi!..."

"Kwani umenisikia?" Nilihoji

"Eeee, wote tumekusikia kasoro baba tu yeye hajarudi, tulijibanza kwenye korido"

"Namshukuru Mungu, lakini naamini ukinifundisha wewe, nitahifadhi kwa haraka zaidi" nilichombeza kwa sauti ya chini kidogo

"Mmh, makubwa" alisema huku akaondoka kwa kuwa mlango mkuu ulikuwa unasukumwa.

Aliyeingia alikuwa mzee Burhani.

"Assalaam aleikum yaa Jamaal" alinisalimu huku akiingia mle chumbani

"Wa aleikum salaam" nilimjibu.

"Sasa leo tujifunze namna ya kusalimia kwa kirefu" mzee alianza somo lake lisilo rasmi...

"Assalaam aleikum wa rahmatullah wa barakatu, hii ndiyo salamu bora kwa waja kusalimiana" aliendelea

"Maana yake ni kwamba, amani ya iwe kwenu na rehema za Allah na baraka zake" aliendelea

"Kujibu kwake ni, wa aleikum salaam wa rahmatullah wa barakatu, na maana yake ni kwamba, nanyi iwe kwenu hiyo amani, na rehema za Allah pamoja na baraka zake" kisha akaendelea.

"Kusalimia ni sunna, yaani ni jambo tulilohimizwa kufanya na ambalo Mtume (rehema na amani zimwendee) alikuwa akifanya" kisha akaendelea...

"Kujibu salamu ni fardhi, fardhi maana yake ni wajibu, hivyo ukisalimiwa ni wajibu kurudisha salaam. Usiporudisha unapata dhambi. Lakini usiposalimia hupati dhambi japo utakosa faida nyinginezo kama utakavyofundishwa siku za usoni" alimaliza na Yasir akawa anaingia...

"Haya, andika herufi zote kwa kufuatisha kama zilivyo kwenye kitabu, hakikisha unaziumba vizuri" Yasir aliniambia baada ya kusalimia.

Wakaniacha nikaendelea na uandishi, haikunichukuwa muda kumaliza, maana na herufi 30 tu. Nikawa tayari.

Muda wa swala ya isha tukaenda kuswali, tukarudi, pia siku hiyo nilikula hapo vyakula vizuri laini laini, ilikiwa tambi za nazi, mikate ya boflo na mchuzi wa samaki (koana) na vidubwashika vingine vidogo vidogo.

Mazungumzo yaliendelea, nikajiona ni kama sehemu ya familia ya mzee Burhani.

Saa nne kasoro niliaga na kuelekea nyumbani.

Kidogo kidogo ratiba zangu zilianza kubadilika.

'Maggot' ziendi tena, 'Tazara' siendi, 'Mboye' siendi, Sikinde tu tena Kariakoo ndio mara moja moja nilikiwa nahudhuria nikiwa kijana mwenye utulivu, ratiba za sinema zikapungua pia.
*********

Nilisomeshwa na Yasir kwa siku tatu tu, taarifa zilikija kuwa lori lake lipo tayari hivyo Alhamisi waliondoka yeye na Abdul kuelekea Kahama.

Siku hiyo ya alhamis nilifika kama kawaida kwa mzee Burhani majira ya saa kumi na nusu hivi, nilikaribishwa vizuri na mama mkubwa, kisha nikaingia chumba cha kusomea.

Mara mama Warda (mama yake Hamida pia) akaingia na kuniambia kuwa Yasir amesafiri leo, hivyo durusu aliyokufundisha, mzee akirudi atakufanyia utaratibu upate maalim wa kukuendeleza.

Nilimjibu kuwa hakuna neno, nitajitahidi kusoma kwa bidii.

Da, nakumbuka siku hii nilisoma kwa sauti ya juu kidogo ili walio vyumba vingine wasikie kama kuna sehemu nakosea basi wanisahihishe.

Nilisoma mara kadhaa na kumaliza nilipoishia na kurudia tena na tena, baadaye Hamida akaja na bilauli...

"Nimekuletea kinywaji kingine leo, ni juisi ya furusadi" alisema Hamida huku akinipatia...

"Bila shaka umeiandaa wewe" nilisema huku naipokea

"Hapana, hii aliandaa mama, mie leo nilitika kidogo, nimerudi muda mchache kabla hujafika" alijibu

Kisha akaendelea...

"Halafu nimekusikiliza kuna sehemu unakosea kutamka..., siyo zwadi, ni dhwad, tamka kwa kujaza ulimi mdomoni..."

"Dhwad" nikajaribu,

"Enheee, hivyo umepatia" akaendelea

"Sasa rekebisha matamshi kwenye fatha'a, na fatha'a ten an, yaani kwenye dhwad."

Nikajaribu, nikaweza, akanipongeza kisha akaketi pembeni yangu kwa nyuma kidogo wote tukiangalia uelekeo mmoja na kuniamuru nisome kuanzia mwanzo...

Nikawa nasoma, na kila nilipokosea ananirekebisha papohapo...

Hali iliendelea hivyo hadi baba yake akaja na kukuta ananisomesha vizuri, akaingia akatuangalia kisha akatoka kwenda sebuleni.

Naye hakukaa muda mrefu akaenda sebuleni, mie nikawa naandika ili yakae vizuri kichwani.


Ahamis ile ilipita vizuri. Niliamua 'kumuua' Hamida kwa kutumia 'sumu ya kuua taratibu', sikuwa na papara na sijui uvumilivu ule ulitoka wapi!

Kuanzia Ijumaa hadi Jumapili ilikuwa siku za mimi kupumzika kufundishwa masomo ya dini, hivyo nilipanga Ijumaa hii niende sinema.

Sikuwa napata nafasi ya kuongea na Hamida nje ya nyumbani kwao, tena akiwa amejihifadhi mwili wote kasoro sehemu ya uso, lakini nilikuwa nafurahia uwepo wake karibu nami hasa siku ya 'jana' ambapo alipokuwa akinirekebisha kusoma vizuri.

"Hivi wewe kwani huwa huendi matembezini? Mie kesho usiku nitaenda sinema Cameo kuna filamu nzuri nimeona kwenye gazeti. Kesho Ijumaa nikitoka kazini nitakuja kununua juisi, bila shaka nitakukuta angalau nikuone maana kesho hadi Jumapili nilichaguwa kupumzika na kufanya mambo mengine"

Hili lilikuwa ni shambulizi dogo na hafifu lakini lenye sumu inayoweza kuua taratibu, ni barua (memo) niliyompatia Hamida kabla hajaondoka kwenye kile chumba kuelekea sebuleni.
*********

Ijumaa nikiwa kazini nilimuaga Marry kuwa naelekea msikitini. Nilitoka saa sita kamili kuelekea maeneo ya mtaa wa mkunguni kisha nikaenda msikiti wa Manyema.

Miaka hiyo maeneo ya mtaa wa Living stone, mkunguni ilikuwa imechangamka sana, katika harakati zangu nilikuwa naonekana maeneo ya kjiwe cha mabaharia (sea men's coner), enzi hizo kazi ya ubaharia ilikuwa ya ujiko sana kwa vijana na wengi walijifunza kuzamia meli (stowaway) kutokea kijiwe hicho... Biashara za jeans kali (used), bidhaa zingine za 'mamtoni' (nje ya nchi) zilikuwa zinafanyika maeneo hayo , siyo kwa maduka maalumu bali mkononi tu, unapata info, Baharia fulani anauza cheni za gold apate nauli arudi 'Belgium', unamvizia, unampa hela anakupa cheni, ama bidhaa nyingine kama alivyotangazia 'wasela' (sikuhizi mnasema masela), Sela lilitokana na ubaharia, Sail, Sailer yani baharia hususan wale wa vyombo vitumiavyo upepo kama nguvu ya kusafirisha chombo (Jahazi, Dau, Mashua, na ngalawa)

Mabaharia wengine walikuwa wanashinda pale Forodhani Atiman House (barabara ya Sokoine na Kivukoni)

Maeneo hayo (Mkunguni / Living stone) kulikuwa na biashara zisizo rasmi za kubadilisha hela yetu na kuwa dola, madini, udalali na kadhalika.

Nikiwa maeneo hayo mida ya waislamu kuswali nilikuwa nasikia adhana kwa ukaribu na pia mawaidha wakati mwingine unayasikia hata ukiwa mita kadhaa kutoka eneo la msikiti, hivyo nilichaguwa msikiti wa Manyema kusalia swala za Ijumaa.

"Hongera, umekuwa mswaliina, katuombee na sisi" alisema Marry wakati natoka

"Ahsante, nitarudi saa saba na nusu hivi maana leo ni siku ya kusikiliza hotuba mbili za Ijumaa" nilisema na kuongeza maneno kidogo kuonesha kuwa dini imeanza kunikolea.

Marry alitamasamu, mie nikaondoka.

Marry kama nilivyozoea kumwita alikuwa ni mtu wa kutoka Kilimanjaro, ana mume na watoto wawili. Nilimzoea sana, lakini sikuwahi 'kumtokea' (kumtongoza) licha ya yeye kunionesha dalili zote za kutaka 'nitembee naye', dalili zilikolea pale naye aliponishirikisha mambo yake ya nyumbani... Hakuwa na ndoa yenye furaha..., ila kuna siku alinitega sana hadi uzalendo ukanishinda, ilikuwa kabla ya kumuona Hamida.

(Stori yake ni fupi sana, nitaelezea kwenye uzi wa kula kimasihara pamoja na stori nyingine ya shindano la kufikisha bao 12)

=

Baada ya Ibada ya Ijumaa nilirudi ofisini kumalizia siku.

"Umependeza kweli na kanzu yako" alisema Mary wakati naingia ofisini huku nimevaa kanzu juu ya nguo nilizovaa asubuhi, kabla sijaenda msikitini, nilipitia Kariakoo mtaa wa pemba kwenye duka moja hivi la mhindi nikanunua kanzu na kofia ya mkono (waliziita kofia za Zanzibar) ndio nikaelekea Manyema.

"Ahsante Marry", nimeamua kubadilika, karibu nawe nianze kukuona ukivaa baibui (buibui), nilisema kisha nikaingia ofisini kwangu.

Enzi hizo mabaibui yalikuwa tofauti na ya sasa, yalikuwa kama yana kikofia hivi (ushungi) halafu lazima ukivute upande mmoja ukibane kwapani kuepuka kulikanyaga ama kuburuza (ilikuwa ndio fashen), rangi nyeusi tii, 'texture' nzuri ajabu. Ilikuwa ni kawaida kwa wanawake kuvaa hayo mabaibui wakitaka 'kutoka' (yaani kwenda sehemu)
********

Marry alicheka akionesha (kwa kumaanisha) kuwa ni vigumu yeye kubadili dini.

Mezani nilikuta bahasha (barua) kutoka wakala la pijot. Saa tisa na nusu nilitoka ofisini moja kwa moja hadi nyumbani pamoja na mambo nipate kuisoma vizuri ile barua
******

Wakati nipo mwaka wa mwisho Uingereza niliwaandikia Peugeot Ufaransa nikitaka wanipatie profoma invoice ya kununua 504 GL pickup. Walinijibu kuwa nipitie wa wakala waliomuidhinisha aliyepo Dar es Salaam.

Hivyo nilivyofika Dar kutoka masomoni nilinunua Batavuz kwa jamaa mmoja wa kutoka Zanzibar pale Mkunguni, ilikuwa kama mpya tu, kisha ndio nikaenda Peugeot house pale mtaa wa Ali Hassan Mwinyi (Bibi titi / Ohio) nikaagiza kupitia wakala wao. Masomo ya post graduate diploma hayakuwa yananichukulia muda sana hivyo nilifanya kazi za part time na kutengeneza hela ya kutosha kununua gari na mazagazaga mengine...

Meli zilikuwa zinachelewa sana kuwasili kutoka ulaya hasa zile zinazozungukia Atlantic hadi South Africa kisha ndio kuja mashariki ya Africa, zile zilizopitia upenyo wa Gibralta kisha upenyo wa Suez zilikuwa zinawahi.

Kwenye ile barua niliambiwa gari yangu imeshafika na ipo afisini kwao hivyo niende kukamilisha taratibu zingine ili nikabidhiwe...

Nilifurahi sana, nikajisema hili litakuwa jambo la kwanza siku ya jumatatu.

Saa kumi na nusu nikaenda kwa akina Hamida, baada ya Mama Warda kunikaribisha nilimuambia leo sikai, sina kipindi bali nilimuagiza juisi Hamida..

"Hamidaaaa" mama Warda aliita huku yeye akirudi sebuleni na kuniacha nimesimama kwenye karido...

"Abee mama" aliitikia Hamida kwa sauti yake nyororo kama ya mama yake, sauti inayonifanya niwe 'mgeni' nyumbani kwao kila siku...

Hamida alitoka chumbani kwake, aliponiona tu, alirudi ndani tena kisha akatoka na kuelekea kwenye jokofu kubwa kuchukuwa juisi niliyomuagiza...

Lengo halikuwa juisi bali majibu ya barua (ki-memo) nilichomuachia jana...

Mapigo ya moyo yananidunda kuliko kawaida, nawaza sijui atajibu namna gani...

Alikuja uelekeo wangu, kwa mwendo wa madaha (ndio mwendo wake ) shingo upande kidogo mikono yote ameshika dumu la lita 3 japo angeweza kulishika kwa mkono mmoja..

Alinikabidhi lile dumu kwa mikono yote miwili na mkono wake wa kushoto akiwa amebana karatasi ndogo ambayo haionekani kwa urahisi, akanigusa vidole vyangu vya mkono wa kulia wakati napokea dumu kama ishara ya kutaka kunipatia kitu...

"Haijaganda sana leo..." Alisema huku ameinama chini kidogo, nami nikamjibu kuwa haina neno nikapokea, nigaaka kwa sauti kubwa ili mama na wengine sebuleni wasikie kisha nikatoka.

Wakati ananigusa vidole nilijisikia kama nimepigwa shoti hivi na kusisimka hatari, nikijikaza kwa kutoonesha tofauti.

Nilitoka hadi nyumbani tena na kuanza kuisoma.

Aliandika mwandiko 'mduchu' sana (what we call microscopic words), karatasi ilikuwa ndogo sana na alitaka kuandika mengi...

Mwandiko umelalia kushoto, nafikiri alitumia zile pen aina ya bic zenye rangi ya njano kwa nje (0.6mm)

Kimemo chake hakikuwa cha mahaba, bali aliandika...

"Assalaam aleikum, mie sijambo alhamdulillah. Jana nilisoma ujumbe wako, huwa natoka lakini kwa sababu maalum ambayo wazazi wataielewa, angalau wakati nasoma nilikuwa huru kidogo, lakini maisha yetu ni ya kufungiwa ndani muda mwingi. Nakuona kuwa una busara kuna jambo mie pia nataka nikushirikishe unishauri, maana hapa Kaka yangu baba na mama wote sioni kwa hiki kama wananishauri vyema. Kesho ukija kurudisha dumu nitakuwa nimeshajuwa namna ya kutoka tuweze kuongea, wa billah tawfiq."

Nilirudia kuisoma memo ile kama mara 23 hivi

Ilikuwa inaniondoa wasiwasi, inatuliza mtima, inaondoa joto, inaleta matumaini kwenye harakati zangu za kuongeza dozi ya 'sumu' maana mzee Katibu Kata alinishauri nisiwe na papara la sivyo nitafeli na kujiaibisha.

Kwa siku moja nilipokea barua mbili zenye kunipa furaha, asikwambie mtu, nikikuwa na furaha sana hasa kile kipengele "kesho nitakuwa nimeshajuwa namna ya kutoka..."
******

Baada ya chakula cha jioni nilienda Cameo Cinema kuangalia filamu mpya iitwayo Grease. Ni filamu ya stori ya mapenzi.

Muda wote nikiwa naangalia sinema hiyo nilikuwa najiona kama mimi ndiye Danny Zuko (Starring) na Sandy ni Hamida....

Nilifurahia sana filamu hiyo na kutamani kama Hamida angekuwepo ukumbini siku hiyo.

Tulifurahishwa pia kwa trela za "bad spensa"

Saa tano na nusu usiku tayari nilikuwa nyumbani, filamu za kizungu mara nyingi huchukuwa dakika 90 ama 120.

Nililala kwa furaha siku hiyo huku nikiona kama saa haziendi ili niende kwa Hamida kurudisha dumu la juisi
****

Majira ya saa tano asubuhi nilienda kwa akina Hamida, bahati nzuri ni yeye aliyenipokea na kunikaribisha sebuleni.

Niliwakuta mama wa kiafrika, mama Warda na Nadya pia wakiwa wanasogoa (wanazungumza)

Hamida alipokea lile dumu kisha akaenda nalo, huku akiniambia...

"nimekutengenezea togwa, najuwa unalipenda, leo ma-mkubwa nilimuambia apumzike, ngoja nikuletee..."

Punde si punde alirudi akiwa na dumu dogo lingine la lita moja lenye togwa ndani, wakati akija nami nilikuwa naaga ili nitoke tukutane kwenye korido.

"Najuwa utalipenda bila shaka, ma-mkubwa alinifundisha vizuri.." Alisema kwa sauti ili wa sebuleni nao wasikie...

"Ahsante, nashukuru ila mie sikai tutaonana kesho ama Jumatatu..." Nilisema huku nikiipokea memo yake nyingine aliyoibana kama jana.

Niliipokea kisha kiganja changu nikashika vidole vyake kwa sekunde kadhaa, akavivuta kujitoa lakini si kwa hasira, akanifungulia mlango. Matendo hayo yalifanyika ndani ya sekunde chache wakati wa kubadilishana yale maneno ya kuagana.

Nilimuaga kwa kumpungia mkono na kuondoka kuelekea nyumbani.
******

=

"Assalaam aleikum, panapo majaaliwa kesho baada ya kunywa chai nimeaga nitaenda Msasani kwa Shangazi, basi kama una nafasi naomba unisindikize nipate kukueleza yanayonisibu, saa nne asubuhi unisubiri kituo cha Mwanamboka Kinondoni, usikose, wabillah tawfiq"

Hayo yalikuwa meneno kwenye memo ya Hamida.

Ikumbukwe kuwa hadi sasa Hamida sijamtongoza na hajui kiasi gani nimempenda na maamuzi magumu niliyofanya na ninayoendelea kuyafanya.

Jumamosi hii ni siku yangu ya kwenda DDC Kariakoo kwenye dansi, lakini ratiba za ibada nazo zinanibana, hivyo nilienda kwa kuchelewa, na safari hii nilikaa upande ule wa watu waliotulia. Madaraja hadi ndani ya kumbi za starehe.

Bahati nzuri Mziki wa DDC Mlimani Park ulikuwa haujaanza, kulikuwa na maonesho ya Kibisa ngoma troup.

Kwenye kikundi hiki ndipo nilipomuona kijana Amri Athumani ambaye alikuwa akiliza watu sana kwa uigizaji wake, hususani igizo aliloigiza kama mtoto wa kambo aliye lelewa kwa manyanyaso na mateso makubwa lakini baadaye alifanikiwa kuwa na maisha mazuri... (Pumzika kwa amani King Majuto)
************

=

Saa zikawa haziendi, enzi hizo hakuna simu za mkononi, hakuna mitandao ya internet, nilisoma masomo ya kutumia tarakikishi (computer) nikiwa Uingereza, naikumbuka pc yangu chuoni ilikuwa IBM 386 ikitumia mfumo endeshi (operating system) microsoft windows 3.1, hadi nacheka hapa, ilikuwa ni ya kisasa sana wakati huo....

Mzee Burhani alikuwa anayo simu ya mezani, lakini sikuwa na tabia ya kuwapigia. Na hata nikimpigia Hamida kwenye simu ya mezani nitaongea naye vipi maneno ya mapenzi akiwa sebuleni na mara nyingi panakuwa na watu...

Njia zilizobakia ni kuonana naye ana kwa ana ama kuandikiana barua.

Sasa kwa memo ile ya Hamida muda ndio ukawa 'hauendi' kabisa!

Niliamua kufanya kazi zote nizifanyazo Jumapili ili siku hiyo niwe huru, nikapaweka vizuri chumbani, sebuleni na mazingira ya nje, nilikuwa msafi kupitiliza, na kazi nyingi nilikuwa nafanya mwenyewe, mwili wangu ulikuwa umejengeka vizuri, nyama nyama zilikuwepo kidogo siyo kama ilivyokuwa miaka sita iliyopita.
*****

Usiku baada ya kula ndio nilienda DDC kwa ajili ya mziki wa dansi.

Baada ya Kibisa ngoma troup kumaliza maonesho yao ya ngoma za asili, mziki wa dansi ulianza taratibu kwa mpiga solo mmoja kuanza kuchombeza... Kisha wanamziki wengine wakachukuwa nafasi zao na burudani ikaanza kuchanganya.

Tulifaidi sana kusikikiza, kucheza na kuwaona mubashari wanamuziki... Upangiliaji wa vyombo, mpangilio wa sauti, maudhui, solo guitar kusikika vizuri, ridhim (rhythm) guitar kusikika bila kumezwa, bass guitar kuchombeza ipasavyo, organ kuchukuwa nafasi yake, saxafone na trumpets kusikika wakati muafaka, drums kuongoza mziki mzima, uchezaji wa wanamziki na wapenzi wa muziki na kadhakika ni burudani safi kabisa iliyotufanya tufurahie na kutokosa kila weekend...
*****

Nitaweka wimbo mmoja kwenye attachment ili wewe kijana wa sasa usikilize kwa makini...

=

Siku ilipita hivyo, nilirudi nyumbani nikiwa mwenye furaha na kupumzika.

Saa mbili asubuhi alarm iliniamsha, nilipitiwa na usingizi hata ibada ya swala asubuhi sikufanya.

Niliamka na kufanya yapaswayo kufanywa asubuhi kisha nikatengeneza chai ya maziwa ya BB condensed milk, slesi za mikate na mayai ya kukaanga.

Saa tatu kamili nipo tayari, nikachukuwa ile memo tena na kuanza kuisoma upyaaaa kama vile sijaisoma....

"...saa nne uwepo Mwanamboka.... Usikose..." Nilijikuta nafurahi kwa mara nyingine tena japo si kwa mtoko wa kimapenzi, kwanza Hamida hajui kama 'nimekufa nimeoza juu yake' nilijisemea.

Nilachukuwa juzuu na kudurusu herufi hadi nilipoishia Alhamisi ili nipate sehemu za kumuuliza ama sababu za kuanzia kuvunja ukimya rasmi...

Saa tatu na robo nilianza safari mdogo mdogo hadi magomeni kituo cha taksi, sikuchukuwa batavuz, nikakodi taksi hadi Kindondoni, akanishusha kituo cha Mwanamboka.

Saa nne kasoro kumi mie nipo kituoni. Nilisimama tu hapakuwa na benchi wala kivuli cha paa.

Hali ya hewa ilikuwa si joto wala baridi, watu wachache barabarani, wengi wao bado wapo makanisani...

Kila baada ya dakika najikuta naangalia motima (saa) yangu, muda hauendi! Mara saa nne hii hapa! Hakuna dalili ya Hamida...

Ilipofika saa nne na dakika ishirini na tano hivi nikaona UDA ya kwenda Mwenge imesimama na kushusha abiria, ilikuwa basi kubwa, na abiria wote walikuwa wakishukia mlango wa mbele, mlango wa nyuma ulikuwa wa kuingilia tu. Na ukiingia tu unakutana na mkatisha tiketi (amekaa) anakukatia kwa mashine flani hivi ndogo kama efd kwa sasa ila ilikuwa mechanical. Kupanda kwenye basi ni kwa foleni.
****

Mara paap nikamwona Hamida anashuka mlango wa mbele na kuja upande wangu...

Alikuwa amevaa gauni la rangi ya pink, mtandio uliofungwa vizuri wa rangi pink, viatu fulani vinavyoziba vidole vya mbele hadi nusu mguu vya pink, mkononi ameshika begi dogo la mkononi nalo rangi ya pink, hakika mavazi yalimpendeza.

"Assalaam aleikum" alinisalimia bila kunipa mkono.

"Wa aleikum salaam Hamida", umechelewa

" Nisamehe, nilichelewa kuaga maana nimebadilisha ilikuwa nirudi baadaye magharibi lakini nimeomba ruhusa nilale huko Msasani, nimekubaliwa" alijibu.

"Batavuz yako umeiweka wapi" aliuliza huku akiangaza huku na huko

" Aaa, leo sikuja nayo, nimekuja kwa teksi" nilijibu

"We nawe, pale na hapa tu unapoteza hela kwa teksi" alisema huku akimaanisha

"Kwakuwa sijui mazingira tuendako ndio nikaona bora niiache ili tutumie usafiri wa jumuiya ama teksi" nilijibu kwa kujiamini.

Nami siku hiyo nilikuwa nimepigilia hasa, nilivaa safari buti, kadet, shati pia kadet, kichwani nywele nimechana vyema (mchicha / afro).

"Nisubiri ngoja nikachukue teksi" nilisema huku naondoka

Dakika chache tu nilirudi nikiwa ndani ya teksi siti ya nyuma upande wa kulia...

Niliinama na kumfungulia mlango...

"Karibu, twende!" Nilisema naye akatii na kuingia kwenye teksi.

"Kituo cha kwanza wapi?" Nilimuuliza Hamida ili atoe ramani kwa dereva

"Katuache Morogoro super market" alidakia Hamida...

Moyoni nikashangaa, mbona tunaelekea huko badala ya Msasani... Ila sikumuuliza.

Kulikuwa na ukimya fulani hivi hadi dereva alipoweka mziki wa Boney M, Dad cool.

Nikaanza kutingisha kichwa, Hamida ananiangalia tu katulia.

Tulivyofika Moroco dereva akapinda kulia na kufuata Bagamoyo road kuelekea mjini (siku hizi inaitwa Ali Hassan Mwinyi rd, tulivyofika mbuyuni mbele kidogo dereva akachukiwa njia ya kushoto barabara ya Haile Selasie moja kwa moja hadi Morogoro supermarket.

Nikamlipa dereva ujira wake kisha tukashuka, Hamida akawa anaelekea ndani ya supermarket, nikamfuata, nikamuuliza mbona tumekuja hapa, akanijibu anataka amnunulie shangazi yake zawadi, hivyo tukaingia ndani kwa ajili ya shopping.
*************


"Samahani kaka, nilikuona kuwa una busara ndiyo maana nilikuomba unisindikize ili nipate kukusimulia yanayonisibu hivi sasa, maana sina wa kuongea naye kwa pale nyumbani kwa hili zaidi ya ma-mkubwa ambaye naye hayupo huru sana kwakuwa mama ni boss wake"

Hamida alianza 'kufunguka' akielezea kisa chake, tulikuwa bado tupo maeneo ya supermarket kwa pembeni kulikuwa na sehemu ya kukaa na kupata viburudisho baridi kama ice cream ama vinywaji baridi, kahawa chai na kadhalika.

Nilikuwa namsikiliza kwa makini huku nikijitahidi kuonesha uso wenye busara muda wote. Tulikuwa tumekaa kwa kuangaliana huku tukiwa tumetenganishwa na meza ndogo.

Kwa mara nyingine hapa nilimfaidi Hamida kwa kumuangalia usoni bila wasiwasi (bila kuibia) na kuona uzuri alionao. Naye wala hakuwa na hofu yoyote juu yangu aliendelea kutiririka...

"Mie ndio kwanza nimetoka chuo Kenya, nilikuwa campus ya Mombasa KUC kwa masomo ya diploma ya miezi kumi na minane, nilimaliza Jangwani girls mwaka majuzi."

"Sasa wiki mbili zilizopita ililetwa posa kwa baba, nikiposwa mie, posa ilitoka Oman. Dada yangu Sabra naye ameolewa huko huko. Sasa tatizo siyo posa maana mie tayari nimeshakuwa, nahitaji kuanza maisha yangu, lakini shida ipo kwa mhusika wa posa yenyewe, mie simpendi..."

Alimeza mate kisha akaendelea....
****

Hapa nilikuwa nafaidi vitu vingi, kuwa karibu naye, alikuwa ananukia uturi mzuri sana, udi si udi, misnk si misnk lakini ni harufu iliyotulia na kutamani kuendelea kuinusa muda wote...
****

"Simpendi kwa sababu anaonekana yupo umri kama wa baba, yani mbabu haswa.."

Alisema kwa kusisitiza huku akiingiza mkono mmoja kwenye mkoba wake na kutoa bahasha ya khaki, ndani yake akatoa picha mbili, moja full size na nyingine ni half size (siyo passport size lakini)

"Hebu ziangalie hizi picha..."

Akanipatia, nikaziangalia kwa makini na kuona kuwa ni kweli asemacho Hamida.

"Enhe, sasa wazazi wameamuaje?" Nilidadisi

"Baba, mama na kaka wote wanataka niolewe, mama Fungameza haoneshi upande wowote, lakini najuwa yupo upande wangu maana naye ndoa yake ilimsumbua sana hadi aliomba talaka na kurudi kwetu.

" He kumbe!" Nikijifanya sijui...

"Ndiyo, mie nimezaliwa nimemkuta ma-mkubwa yupo kwetu, tuko naye miaka mingi" aliongeza kisha akaendelea...

"Baba anasema mara oooo, yule tajiri kwao huko, mara oooo, tuna udugu naye kiukoo mara oooo eti nitakaa na dada yangu mji mmoja, yani vijisababu ambazo mie hata sizikubali" aliongea huku kwa mara ya kwanza nilimuona anabinua mdomo kwa kuonesha hasira zake (bila kudhamiria)

"Sasa kali kupita yote eti mie niwe mke wa tatu, yaani pale alipo ana wake wawili mie binti mdogo hivi nikawe mke wa tatu, aku, bikra yangu nitamzawadia nimpendaye" alisema huku akionekana kuchukizwa

"Kwani dini inasemaje kuhusu uke wenza na kuolewa na mtu mzima, maana mie ndio kwanza najifunza, nawe ni mwalimu wangu..." Nikatabasamu kidogo kisha akadakia...

"Kidini wala si haramu, mtu waweza kuoa ama kuolewa na mwenza wa umri wowote ili mradi mume aweze kutumiza mambo manne muhimu kwa mke..."

"Enhe, yapi hayo mwalimu wangu" nilimuuliza

"Mie siyo mwalimu wako, mzee Burhani atakutafutia, mie nimekusaidia tu pale ninapopajuwa..." Alisema

"Ndiyo mwalimu wangu tena, hata kama umenifundisha kipindi kimoja" nilisema huku nacheka kwa mbaaali.

"Jambo la kwanza ni kuweza kukidhi haja ya ndoa kwa maana ya jimai" alisema

"Hebu fafanua hapo wala sijaelewa..." Nilimuuliza, akainama chini kidogo na kusema...

"Awe na uwezo wa kufanya tendo la ndoa, jimai ni tendo la ndoa"

"Ahaaaa, enhe?!" nilielewa sasa nakumuache aendelee...

"Jambo la pili ni mume awe na uwezo wa kumlisha mke" kisha akasita kidogo halafu akaendelea

"Yaani aweze kuhemea (kutafuta) na kuleta rizki halali nyumbani kwa ajili cha chakula" alimaliza

"Hapo sasa nimeelewa maana nilitaka kukuuliza swali la ufafanuzi" nilichagiza.

"Muoaji pia awe na uwezo wa kumvisha mke, yaani aweze kumpatia nguo kiasi cha kumsitiri maungo mkewe" alitulia kisha akaendelea...

"Jambo la nne ni aweze kumpa malazi mkewe, yani awe na sehemu ya kulala., hayo ndiyo mambo manne muhimu yatakiwayo" alimaliza.

"Ahaaa, sasa mchumba wako anakosa lipi kati ya hayo?" Nilimuuliza

"Kwa maelezo ya baba inaonekana yote anaweza kutimiza lakini mie siiweki rehani bikra yangu kwa mbabu, nijitunze weeee kisha niangukie kwa babu, tena uke wenza!" Aling'aka.

"Kwani uke wenza si inaruhusiwa kwa dini yetu?!" Nilionesha kuiva kwa imani.

"Ndiyo, inaruhusiwa lakini mie hata sikubali, ningekuwa tayari nimeshaolewa na kuachika labda ningekubali, ama ningekuwa mjane labda..."

Alitulia kisha akaendelea

"Ndiyo naenda kumwambia Shangazi nione naye atasimamia wapi" alimaliza.

"Du, pole sana" nilimpa pole huku nikimrudishia zile picha.

"Sijapoa bado, ndiyo maana nimekuomba uje unisikilize kisha unishauri" alisema na kushusha pumzi ndefu kisha kutulia.

"Eee kweli, hili jambo ni zito kwako, na linahitaji busara kubwa katika kuliendea"

Nilisema kama mshauri vile kumbe nami ni mmoja wa waposaji watarajiwa, nilikuwa napima tu anapenda nini na vitu gani.

"Kwani wewe katika makuzi yako hukuwahi kupata boyfriend uliyempenda, ili umwambie aje atoe posa nyumbani?" Nilimuuliza huku namuangalia kwa makini usoni.

Akawa anafikisha vidole huku ameinama kiasi na kusema...

"Wakati nipo form two, kulikuwa na mwanafunzi wa Almuntazir wa A-level, alikuwa ananipenda sana, tulikuwa tunakaa wote Magomeni, yeye alikuwa akiishi mtaa wa suna, alikuwa ana baiskeli nami nilikuwa nayo hivyo mara nyingi tulionana njiani, akajenga mazoea, Jangwani nzima walikuwa wanadhani nimetembea naye lakini ukweli ni kwamba hatuwahi kufanya lolote zaidi ya barua za mapenzi, ila aliahidi akimaliza masomo ya chuo atakuja kuniona. Lakini bahati mbaya alifariki kwa ajali ya gari. Baba yao alikuwa na kiteksii datsun cha mashindano ndio walikuwa wanafanya mazoezi kwa ajili ya mashindano ya Safari Rally yaliyofanyika mwaka juzi, aliumia vibaya sana kwa ajali, mgongo ulivunjika, alipelekwa India kwa matibabu zaidi lakini mwaka jana alifariki" alikatisha huku machozi yakimtoka bila kujuwa.

"Ooh masikini, pole sana Hamida" Nilisimama na kumfuata na kumkumbatia kwa nyuma yeye akiwa bado amekaa na kuinama, kisha nikampa handkerchief.

Pakawa na kimya fulani hivi kisha nikakata ukimya kwa kuendelea kumshauri...

"Pole sana Hamida, Mungu amuweke mahali pema peponi amin" nilisema na kumuuliza...

"Hakukuwa na mwanmume mwingine aliye kutaka ama kukuposa?"

"Wanaonitaka wapo wengi tu, sisi watoto wa mzee Burhani tuna sifa ya tabia njema kule mtaani, tuna malezi bora ya kiislamu..." Akasita kidogo kisha akasema

"Ila sasa nami nimechoka kukaa ndani nataka nianze maisha yangu..."

"Sisi mara nyingi tunaolewaga wenyewe kwa wenyewe, Dada yangu Warda ameolewa Mwanza kwa baba yetu mwingine, Sabra naye Oman kwa ndugu mwingine, lakini yeye angalau mumewe amemzidi miaka sita tu..."

Alijifuta usoni vizuri kwa kitambaa kisha akaendelea...

"Hivyo kwa kujibu swali lako ni kwamba hakuna, labda mbabu wa Oman... Hahahhaha" akacheka.

Sasa ikabaki zamu yangu ya kumshauri. Nitamshauri nini zaidi ya 'kuvutia ngozi' upande wangu!

"Okay, sasa wewe uende kwa Shangazi, mueleze yote, utapata busara zake, nami nipe muda kidogo hadi Ijumaa ijayo nitakupa majibu muafaka wa namna bora ya kukwepa usilotaka." Nilimaliza kibaharia namna hiyo.

Akanishukuru sana kwa ushauri wangu, tukainuka na kuita teksi ili itutoe pale...

"Tupeleke mtaa wa Kimweri na Ghuba Msasani" alisema Hamida

Dereva aliondoa gari na tukaanza kuelekea huko.

"Hivi kumbe unaweza kuletewa picha ukaambiwa ni mchumba, ukamkubali, kama ni picha ya zamani je!" Nilimuuliza Hamida kuondoa ukimya garini.

"Hapo sasa, maana waoaji wa mbali anaweza kuwakilishwa na mtu aliyemridhia, siku ukienda kwa mumeo unashangaa na roho yako unakutana na kibabu!"

Tukacheka wote kwa pamoja.

Dereva wa teksi naye alikuwa 'mfukunyuku' akaweka kanda ya Robert Nesta Marley, wimbo ulioanza unaitwa Turn your light down low!

Ulipofika sehemu ya kibwagizo nikajikuta nami naimba kwa sauti ya chinichini...

 "....I want to give you some love!, I want to give you some good good lovin'....

" .... Never try to resist oh no!, never never try to resist no more!..."

Pakawa na ukimya tena hadi wimbo mwingine ukaja...

" I wanna love you, and treat you right, I wanna love you and treat you alright...."

"Is this love is this love is this love that I'm feelin...'"

"....Everyday and every night, we'll be together..."

"...We will share the shelter of my single bed, we'll share the same room..."

Yani nikajikuta niko so high, Hamida ametulia kama hasikii kitu...

Baada ya kona mbili tatu tukafika mtaa wa Ghuba jirani na msikiti...

"Mie nashukia hapa"
Alisema Hamida, kisha akaniambia nyumba ya tano kutoka msikitini upande ule ndio kwa dada yake baba"

Alishuka na nikamsaidia kushuka bidhaa alizomnunulia aunt yake.

"Twende Moroco" nilimuambia dereva baada ya kumuacha Hamida pale.

Nilikuwa najuwa kesho Jumatatu tutaonana 'darasani'

Moroco nilishuka, nikasubiri Uda kisha nikarudi hadi magomeni nikaenda straight nyumbani



Siku hazigandi, mara Ijumaa hii hapa nipo kazini na muda wa kufunga ofisi imekaribia...

Nilimuaga Marry na kutoka na Batavuz yangu. Sikuwa napenda kwenda na gari ofisini.

Wiki hiyo yote nilikuwa namuhadithia Marry maendeleo ya mimi na Hamida, akawa ananiambia kweli umedhamiria...

"Atakuweza kweli na nanihii lako kubwa hivyo!" Alisema huku sasa akiwa anaamini kabisa nipo serious kuhusu Hamida.

"Maana mie mwenyewe niliweza kwa tabu japo nimezaa watoto wawili tena kwa kusukuma, lakini shughuli niliipata..."

Aliendelea kusema huku akionesha dalili za kutamani tena. Zaidi ya siku ishirini sasa sijapata msichana wa kustarehe naye, nami wala sikuwa na 'moto' zaidi ya kumuwaza Hamida.
***



ITAENDELEA

No comments