SIRI ZA KUDUMU KATIKA MAHUSIANO YA MAPENZI
Watu wengi wanatamani kudumu kwenye uhusiano lakini bahati mbaya huwa inashindikana. Mtu ambaye hadumu kwenye uhusiano, si kwamba anakuwa hapendi bali inatokea tu kutokana na sababu mbalimbali. Inatokea kwa sababu, huenda pengine ni kutokana na tabia zake au za mwenzake. Mfano, yawezekana akawa na ‘mdomo’ sana, yawezekana akawa mbinafsi. Au ana hulka ya ugomvi lakini mwenzake hana. Yawezekana akawa na tabia za kuchepuka.
Yawezekana tatizo likawa la mwenzake, Akawa ana tabia zisizompendeza mpenzi wake. Yawezekana akawa mbinafsi, yawezekana akawa na hasira kali au akawa na tabia mbaya ambazo mwenzake ameshindwa kuzivumilia. Kikubwa tu, watu hushindwa kudumu penzini kwa kupishana mambo mbalimbali. Kuanzia tabia, mtindo wa maisha na wengine kutoelewana dhumuni la safari yao.
Mara kadhaa nimekuwa nikisisitiza, unapoanzisha uhusiano na mwenzako lazima kwanza mjue lengo au madhumuni ya huo uhusiano wenu. Mwanamke ajue kwamba uhusiano wao ni wa muda mrefu au wa muda mfupi.
Una malengo au hauna? Vivyo hivyo mwanaume, kwa kinywa chake, kutoka moyoni athibitishe lengo na madhumuni ya uhusiano wake ili mwenzake ajue kabisa kwamba yupo kwenye uhusiano wa aina gani. Baada ya hapo ndio muanze safari.
Na hii ndio siri ya maisha. Ndiyo siri ya uhusiano wote. Mkishajua madhumuni ya safari yenu, kinachofauta ni kukipa umuhimu kipaumbele chenu. Pamoja na kujua kwamba mtakumbana na changamoto mbalimbali katika safari yenu lakini mnapokumbuka umuhimu wa safari yenu, mnatiana moyo. Mnapokutana na magumu yasiyokuwa na mfano, hamkati tamaa. Mnainuka na kusimama tena. Kila mmoja anapomuona mwenzake kakosea, anambebea makosa yake na kumsamehe kulingana na uzito wa safari yao.
Ni kama kiapo. Mnaapa kutoachana, mnaapa kuianza safari pamoja na kuimaliza pamoja. Kifo pekee ndicho kitakacho watenganisha kama kweli wote wawili mtakuwa na nia moja, dhumuni moja la kujenga uhusiano wenu hudumu. Wapenda-nao mnapaswa kuzungumza lugha moja. Kwa pamoja mnapaswa kuazimia namna ambavyo safari yenu mnataka iwe. Mathalan, mnataka muishi maisha ya aina gani? Mnataka kufikia hatua au kufunga ndoa ya aina gani?
Ili muweze kufanikisha safari yenu ya ndoa, mnapaswa muishije? Narudia tena, kusikilizana ndio jambo kubwa sana katika safari yenu. Asiwepo mtu wa kumdharau mwenzake. Mwanamke, amthamini mwenzi wake kuliko mtu mwingine yeyote. Mwanaume, amthamini mwanamke wake katika kiwango cha hali ya juu. Asikubali kuyumbishwa na tamaa za kimwili, asirudishwe nyuma na maneno ya watu na kisiwepo kizingiti chochote cha kumkatisha tamaa.
Kwa vyovyote itakavyokuwa, suala lenu la ‘utaifa wa uhusiano’ ndio mlitangulize mbele. Muishi mkijua kwamba, uhai wa penzi lenu mmeushikilia nyinyi wawili. Mna kila sababu ya kulilinda penzi lenu kwa gharama yoyote kwani mafanikio ya uhusiano wenu, ni mafanikio ya wote wawili.
Mpendane. Mheshimiane katika kiwango cha juu. Kila mmoja atambue majukumu yake. Mwanamke amtii mwanaume, amheshimu. Mwanaume ampende sana mwanamke. Asimdharau, atambue thamani yake katika nyumba licha ya kwamba mwanaume ndio kichwa cha familia.
Mwanaume asivimbe kichwa. Amshirikishe mwenzake katika masuala yanayohusu maisha na uhusiano wao. Hata ikitokea mmepishana kauli, shukeni. Kila mmoja aongozwe na busara kwamba, ipo njia mbadala ya kuwavusha kwenye mabishano hayo bila kusababisha mtafaruku.
Mwanamke usiwe mzungumzaji sana kwa mwanaume. Mpe faraja pale inapobidi. Farijianeni katika vipindi mbalimbali mnavyopitia. Muanguke na kuinuka pamoja. Asiwepo mmoja kati yenu achukulie changamoto ya mwenzake kama si yake.
Kila mmoja aguswe na matatizo ya mwenzake. Mnapokuwa kwenye furaha, kwa pamoja pia mfurahi. Msiwe na tamaa. Tengenezeni maisha yenu mnayoyataka. Kwa pamoja mtakuja kufurahia ushindi wa safari yenu.
No comments