Breaking News

Angalia jinsi mahusiano yanavyoweza kuanza wakati wowote pasipo kutarajia

 


Unaweza kushangaa lakini ndio ukweli wenyewe kwamba upo uwezekano mkubwa kabisa wa kuanzisha na kuendeleza mahusiano na mtu yeyote bila kujali mwonekano wake, tabia yake na imani yake. Katika makala haya tunaeleza kanuni za kimaumbile zinazoongoza mahusiano ya watu wawili ambao mara nyingi watu hao hukutana kwa njia ya nasibu. 
Pamoja na imani kwamba mahusiano bora huwezekana kwa kukutana na mtu sahihi, tunaambiwa na watalaam wa mahusiano kwamba mwanamke yeyote anaweza kabisa kuwa na mahusiano na mwanaume yeyote kwa amani ikiwa kila mmoja wao atakuwa 'motivated' kujua mahitaji ya mwenzi wake huyo na kuyajibu ipasavyo. 
Lakini kabla sijaeleza zaidi, nikumbushie mambo makuu matatu tuliyoyaona katika makala ya nadharia ya mahusiano na mapenzi ambayo ndiyo yanayoanzisha mahusiano kwa maana ya kuwafanya watu wawili wapendane. Mambo hayo ni: 
1) Hisia za kimapenzi au tamaa
Ingawa tamaa ina nguvu kubwa sana katika kuanzisha mahusiano, haiwezi kudumisha uhusiano huo kwa muda mrefu. Misingi ya hisia hizi za kimapenzi ni maumbile yanayoonekana. 
2) Urafiki au ukaribu unaojenga mazingira ya watu wawili kuwa karibu kihisia
Tuliona kuwa misingi ya ukaribu huu ni namna gani mahitaji ya kihisia ya mwenzi yanavyotambuliwa na kujibiwa bila kujali urafiki huo umetokana na tamaa au maamuzi na huu ndio msingi wa maamuzi.
3) Maamuzi ya kuweka ahadi.
Ingawa kwa wengi dhamira ya kudumisha uhusiano hutokana na mawili ya awali, wakati mwingine, hutokea maamuzi hayo yakawa chanzo cha kuchipua kwa urafiki na hisia kama ilivyokuwa kwa wazee wetu zamani. Hiki ndicho kiwango cha juu cha uhusiano. 
Sasa, ingawa uhusiano unaweza kuchipukia kokote kati ya tamaa, urafiki na maamuzi kutegemeana na imani, mitazamo na utamaduni wa wahusika, kilicho muhimu zaidi ni kile kinachofanyika baada ya uhusiano huo kuanzishwa ili kuufanya uendelee. Katika makala hii tutafafanua zaidi conditions muhimu za kuupeleka uhusiano huo mbele kama tulivyoahidi. 
Mahusiano yanavyoanza
Kwa kawaida, uhusiano huanza pale mtu anapovutiwa na mwingine iwe kihisia au kimwili. Hiyo ndiyo hatua ya kwanza kabisa ya mahusiano ambayo hutegemea masuala makuu mawili. 
Kwanza kabisa, ni ukaribu, propinquity. Tunaambiwa kwamba, watu wawili wanapojikuta bila hata wao wenyewe kutarajia katika mazingira ya ukaribu iwe kwa kufanya pamoja kazi ofisi moja, kuabudu mahali pamoja, kusoma mahali panapofanana au kuishi mtaa mmoja, huongeza uwezekano wa mmoja wao kuvutiwa na mwenzake na hivyo kuanzisha mahusiano. 
Tafiti zinathibitisha kwamba kadri unavyokutana na mtu iwe kwa kumwona na kumsikia mara kwa mara, ndivyo unavyoongeza uwezekano wa kumpenda (liking) na kwamba kwa kawaida, hatuvutiwi na vitu tusivyojua kwa karibu ikiwamo watu. Kwa maana nyingine, kadri unavyokutana na mtu ndivyo unavyojikuta ukiongeza evaluation ya kumpenda. 
Kwa upande mwingine, ukaribu huu huongeza uwezekano wa kufanana mambo fulani fulani kama imani na mitazamo na hivyo kuongeza ukaribu. Mfano, vijana wanaokutana kanisani mara kwa mara kwenye ibada, mbali na kuongeza uwezekano wa kuvutiana, lakini pia huongeza uwezekano wa watu hao kuwa na imani, mitazamo na interests zinazofanana. Haya matatu huwa ni kichocheo cha mvuto unaojenga mawasiliano ya kimapenzi. 
Jambo la pili linaloanzisha mahusiano ni mvuto wa kimwili. Hapa tunazungumzia uzuri wa sura, urefu/ufupi, unene/wembamba, weupe/weusi na kadhalika. Sasa, uzuri ni relative.  Watu wanatofautiana namna wanavyotafsiri uzuri kutegemeana na utamaduni, malezi, imani na sababu nyinginezo. Na wakati mwingine, uzuri wa mtu hutegemea pia 'viwezeshi' vingine kama mavazi, mapambo, anavyozungumza, anavyotazama na kadhalika. 
Vyovyote vile iwavyo, wengi wetu huamini mtu mwenye mwonekano tunaouona sisi kuwa ni mzuri, basi automatically huwa na haiba na tabia njema. Tuna mazoea ya kuhusianisha uzuri unaoonekana na uzuri usioonekana. Ni aina fulani ya stereotype yenye misingi yake kwenye malezi. Kwamba mzuri ana tabia nzuri jambo ambalo hutufanya tutamani kuhusiana na watu tunaowachukulia kuwa wazuri. 
Hata hivyo, tunaambiwa, pamoja na kwamba watu wengi hutamani kujenga mahusiano na watu wenye mwonekano mzuri wa kimwili, mara nyingi huishia kujenga mahusiano na watu wenye mvuto unaolingana na mvuto walionao wao wenyewe. Unajikuta unahusiana na mtu anayefanana na wewe kwa kiasi fulani. Ni hivyo mara nyingi. Ndio kusema, wanaotamani kuhusiana na watu fulani wenye uzuri wa viwango fulani, hujikuta wakihusiana na watu wa kawaida kama wao. 
Bahati mbaya ni kwamba, mwonekano wa mwili huwa na nafasi kubwa katika hatua za mwanzo za uhusiano na kuwa mahusiano ya kudumu huwa hayategemei mvuto kama nitakavyoeleza katika aya chache zinazofuata. Lakini pamoja na matatizo yake, uzuri wa sura na umbo una nafasi yake, kubwa tu, ya kumfanya mtu ajiingize kwenye mahusiano. 
Mambo yanayoendeleza mahusiano mapya
Wataalam wa mahusiano wanatuambia, baada ya mtu kuvutiwa na mtu fulani, ni kawaida mtu huyo kufanya juhudi za kumvutia mtu huyo kwa kujaribu kujenga taswira chanya ili naye avutiwe naye. Kanuni nne kubwa zinazosaidia kuwafanya watu wawili waanze kuwa karibu kihisia, ili waweze kuhusiana bila mikwaruzo, tranquility, ni haya yafuayo: 
Kwa kawaida, watu hujenga uhusiano na wale wanaowafanya wajisikie vizuri, yaani wanaowafanya wajisikie rewarded. Na kadri mtu anavyojisikia vizuri, ndivyo anavyovutiwa na wewe. Kinyume chake, ni kujisikia mzigo na hivyo kuongeza uwezekano wa mahusiano kwenda mbele. Kwa mfano, mwanamke hujisikia vizuri anapokuwa na mtu anayemfanya ajisikie kuwa mzuri na wa maana kama tulivyoona.
Watu wana kawaida ya kukupa kile unachowapa, hivyo mtu anayeonesha kuvutiwa na sisi, hutufanya tujisikie kuvutiwa nae na kutamani kutumia muda mwingi nae. Tunajisikia kuchoka tunapompenda asiyeonesha kutupenda. Kwa hiyo mtu humpenda zaidi yule anayempenda na yeye. 
Watu unaofanana nao imani, mitazamo na misimamo hupendana zaidi kuliko wale wanaotofautiana imani, mitazamo na misimamo. Kufanana kunakoambatana na mvuto wa kimwili, huchochea mvuto, na mvuto huo huchochea kufanana. Hata hivyo, watafiti wanasema, zipo tofauti za kihaiba ambazo kwa kawaida huchochea kuvutiana. Mfano mtu mzungumzaji hujisikia kuvutiwa (reinforced) na mtu anayeweza kumsikiliza na si yule anayetaka kuzungumza kama yeye. 
Kumwamini unayevutiwa naye, humfanya avutike kwako. Hii hutegemea kiwango cha usalama wa kihisia (emotional security) unachokuwa nacho wewe na kiwango hicho hicho cha usalama anachokuwa nacho yeye. Kutokuwa salama kihisia (insecure) kunamaanisha ama kutokujiamini, kutokuamini wengine au vyote viwili, ambavyo huathiri kwa kiasi kikubwa uhusiano. Unaweza kusoma zaidi kwenye makala haya yaliyopita. Lakini kwa kifupi, nafsi isiyosalama, hushindwa kuamini na hivyo hupunguza kumvutia mwingine.
Sasa je, unaweza kuhusiana na mtu yeyote? 
Jawabu ni ndio. Tafiti zinathibitisha kuwa inawezekana kuhusiana na mtu yeyote anayeweza kukufanya ukajisikia kupata mahitaji yako ya kihisia na kukusababisha na wewe uweze kutambua na kujibu mahitaji yake ya  kihisia kama tulivyoona kwenye makala zilizopita. Kwa muhtasari tu, tunazungumzia namna gani mwanaume anamfanya mwanamke ajisikie kupendwa, na hivyo kuwa na hamasa ya kumfanya mwanamke huyo amfanye mwanaume husika ajisikie mwenye mamlaka. 
Kama tulivyoona awali, ukaribu na mtu hata asiyekuvutia unaweza kuamsha hisia za kuvutiwa kadri unavyoonana nae na namna mtu huyo anavyoweza kuonekana kuelewa na kujibu mahitaji yako ya kihisia. Tunaambiwa, sura unayoweza kuiita mbaya, inapoambatana na jitihada za kutambua na kuelewa mahitaji yako ya kihisia, mitazamo na imani inayofanana na ya kwako, inayokufanya ujisikie vizuri, basi, hatua kwa hatua 'ubaya' wa sura hiyo uliouona awali, hupotea na kugeuka kuwa uzuri. 
Vile vile, namna gani uhusiano unakupa kipimo kinachofanana na kile ulichowekeza kwenye mahusiano na hivyo kujenga hali fulani ya usawa (equity), ndivyo uhusiano huo unavyoimarika na kudumu. Watu hawapendi kuonekana wanagharimika zaidi kwenye mahusiano kuliko huyo wanayehusiana nae. Inawafanya wajisikie kubeba mzigo. Wanashusha ego zao. Ndio maana inapoonekana kuwa huyo unayehusiana naye hana uliochonacho, mara nyingi, humbidi anayepungukiwa kufidia kile asichonacho kwa namna nyingine, ili kumfanya mwenzake ajisikie kuwekeza sambamba na alichowekeza mwenza wake. 
Kwa mfano, mwanaume asiye na elimu, anapoanzisha uhusiano na mwanamke anayemzidi kielimu, huweza kujikuta katika mazingira ya kutokujiamini. Ili ajisikie vizuri, yaani ajiamini, kwa kujua au kutokujua mwanamme huwa na kingine kinachofidia tofauti hiyo ya elimu ili kudumisha uhusiano huo. Inaweza kuwa uwezo wa kifedha, umaarufu na kadhalika. 
Kwa hiyo tunachokisema ni kwamba, inawezekana kuhusiana na mtu yeyote. Na kwa hakika, si kweli kwamba mahusiano bora huwezekana unapokutana na watu sahihi, right women/men. Kama tulivyoona mahusiano yoyote huanza kwa njia ya nasibu, kutegemeana na uliko na unayeonana nae. Kinachowaunganisha watu wawili kimapenzi ni namna wanavyoweza kuelewa na kuitikia ipasavyo mahitaji yao ya kihisia. 
Kwamba, mtu sahihi ni matokeo ya mtazamo, imani na matarajio yako. Mtu sahihi kwenye mahusiano ni wewe na sio huyo unayeonana nae. Kwamba ndio, ukiweza kumnyafanya akufanye ujisikie kupendwa, ni dhahiri unaweza kumpenda na kuishi na mtu yeyote tofauti na wanavyoamini watu wengi.

No comments