Zijue njia 10 za kukufanya kuwa na furaha
Kutokana na changamoto za kimazingira, kiuchumi na kijamii, watu wengi wamejikuta wakikosa furaha. Ni wazi kuwa kukosa furaha kuna madhara makubwa kwenye afya ya mwili, akili na hata katika utendaji wako wa kazi.
Watu wengi hutamani kuwa na furaha lakini bado hawapati furaha; wengi hudhani kuwa na vitu kama vile pesa ndiyo chanzo cha furaha, lakini mambo hayawi kama walivyotarajia pindi wapatapo vitu hivyo.
Je unahitaji kuwa na furaha ili uboreshe afya na ufanisi wa utendaji kazi wako? Karibu nikushirikishe njia 10 za kukufanya kuwa na furaha.
1. Samehe
Watu wengi hukosa furaha kutokana na kubeba uchungu na maumivu yaliyotokana na watu waliowakosea. Ikiwa unataka kuwa na furaha ni muhimu kumsamehe aliyekukosea hata kama hajaomba msamaha.
Kumsamehe aliyekukosea kuna manufaa kwako zaidi kuliko kwa yule aliyekukosea. Mara nyingi aliyekosea huendelea na maisha yake ya kawaida huku aliyekosewa akizidi kuumia.
2. Fanya unachokipenda
“Mafanikio siyo ufunguo wa furaha. Furaha ni ufunguo wa mafanikio. Kama unapenda unachokifanya, utafanikiwa.”
Albert Schweitzer
Moja kati ya siri kubwa ya kufanikiwa na kuwa na furaha katika kile unachokifanya, ni kwa kupenda kile unachokifanya. Unapopenda kile unachokifanya, utakuwa na amani na furaha mara ukutanapo na changamoto au vikwazo.
3. Kuwa na shukrani
Mara nyingi tunatazama mambo mengi kiasi cha kushindwa kuwa na shukurani kwa yale tuliyonayo. Ni rahisi kuona kuwa mambo kama vile afya, marafiki, usalama, malazi n.k. ni mambo madogo ambayo hatupaswi kushukuru kwa ajili yake.
Kwa hakika wapo watu wanaotafuta mambo hayo lakini hawayapati. Hivyo ili kupata furaha ni muhimu kutambua na kushukuru kwa yale machache tuliyonayo.
4. Saidia wengine
Kumsaidia mtu mwingine siyo kumpa pesa au vitu; hata kumpa mtu ushauri au kumtia moyo kunaweza kuwa na maana kubwa kwa mtu huyo.
Unapomsaidia mtu mwingine unajisikia kuwa na thamani na furaha kwani umeweza kufanya kitu chenye manufaa kwenye maisha ya mtu mwingine.
Nakumbuka niliwahi kumshauri mtu mmoja aliyekuwa amekata tamaa kutokana na kukosa pesa; baada ya muda kupita nikakutana naye, akashukuru sana kwa ushauri wangu. Alinieleza kuwa kama siyo yale maneno niliyomweleza angekuwa ameshajiua. Ni wazi kuwa nilijihisi mwenye furaha na amani kutokana na kuweza kumsaidia mtu mwingine.
5. Shirikisha wengine
Inawezekana jambo linalokukosesha furaha kuna mtu mwingine anafahamu utatuzi wake. Hivyo kwa njia ya kumshirikisha mwingine utapata ushauri au hata utatuzi wa tatizo lako. Jambo la kuzingatia ni kuhakikisha unamshirikisha mtu sahihi.
6. Ondoa mawazo hasi
“Akili ni kila kitu. Unavyofikiri ndivyo unavyokuwa.”
Buddha
Mawazo gani uliyonayo kwenye fikra zako? Je unawaza tu huwezi au kushindwa? Mawazo hasi au ya kushindwa ni chanzo kikuu cha kukukosesha furaha.
Amini unaweza hatakama unaona giza; leo ni giza, kesho ni mvua lakini keshokutwa jua litawaka.
Usikate tamaa, ondoa mawazo mabaya yanayokufanya ukose furaha na mani sasa.
7. Usitafute ukamilifu
Mara nyingi watu hukosa furaha kwa sababu wanatafuta ukamilifu. Kwa hakika hakuna binadamu aliyekamilika; wote tuna madhaifu na mapungufu ya aina mbalimbali.
Badala ya kuyatafakari madhaifu yako na kuruhusu yakukoseshe furaha; yakubali na ukabiliane nayo kwa namna bora zaidi.
8. Kaa na watu sahihi
Je umekaa katikati ya watu wanaokulaumu, kukudharau au kukubeza kila wakati? Au pengine umekaa katikati ya watu walioshindwa wanaolaumu na kulalamikia kila kitu?
Watu wa aina hii wanakusababisha ukose furaha. Hakikisha unakaa katikati ya watu wanaokutia moyo na kukuthamini. Epuka watu walioshindwa ambao kazi yao kubwa ni kulalamika na kulaumu kila kitu.
9. Ishi maisha yako
“Muda wako ni mdogo, usiupoteze kuishi maisha ya mtu mwingine.”
Steven Jobs
Watu wengi hukosa furaha kutokana na kuishi maisha ya watu wengine. Jikubali ulivyo, usitake kuwa kama mtu mwingine kwani hutoweza na utaishia kukosa furaha. Tambua wewe ni wa pekee na tembea katika upekee wako huo.
10. Jiburudishe
Je unajua kuimba? Je unapenda michezo au kusikiliza mziki? Kama jibu ni ndiyo, basi hii ni njia mojawapo amabayo inaweza kukupa furaha.
Ikiwa umekosa furaha, unaweza kuimba, kusikiliza mziki au hata kushiriki kwenye mchezo unaoupenda
Hitimisho
Naamini sasa baada ya kusoma makala hii juu ya njia za kupata furaha, hutokosa tena furaha maishani mwako.
Usiruhusu vitu vya dunia hii vinavyopita vikunyime amani na furaha; maisha ni bora zaidi kuliko vitu.
No comments