Breaking News

FACEBOOK CHATTING….6

 

DORCAS: Nyemo. MIMI: (Huku nikijisikia noma moyoni) Naam. DORCAS: nakupenda sana. MIMI: Dah! DORCAS: Nini tena? MIMI: Nikuulize kitu? DORCAS: Uliza.     Kwanza nikakaa kimya kwa muda, kichwa changu hakikuwa kikionekana kuwa sawa kabisa katika muda huo. Ni kweli kwamba nilikuwa nikitamani sana kuwa na Dorcas kwa sababu tu nilikuwa nampenda sana tena toka kitambo, sasa swali ambalo lilikuja akilini mwangu kwa wakati huo, ni kwa jinsi gani alikuwa amefahamu kwamba mimi nilikuwa Nyemo na wakati nilitumia jina langu la A.K.A? Kila nilipojiuliza, nikakosa jibu.   MIMI: Umejua vipi kama ni mimi? DORCAS: Nilikuwa na machale. MIMI: Acha kunitania Dorcas…machale gani hayo yaliyokufanya unitambue? DORCAS: Si kwa sababu ulikuwa unanipenda. MIMI: Si kwamba nilikuwa. Nakupenda mpaka sasa. DORCAS: Nashukuru kusikia hivyo. MIMI: Ila bado haujanijibu Dorcas. DORCAS: Hiyo ni kwa sababu natumia akaunti mbili. Kuna kipindi nilikutumia meseji kwa kutumia akaunti yangu nyingine na kisha kukutumia ombi la urafiki, ukanikubalia. Sasa uliponitumia urafiki kwa kutumia akaunti hii, nikaona ‘matual friend’ akiwa mmoja. Nilipocheki, nikakuta ni akaunti yangu nyingine. Kwanza nikashtuka, sikujua kama nilikwishawahi kuwa na rafiki mwenye jina hilo. Nilipoangalia meseji za kule, nikagundua kwamba ni wewe. MIMI: Mmmh! DORCAS: Nini tena? MIMI: Wewe mjanja sana. DORCAS: Kawaida tu Nyemo. MIMI: Sawa. Ila mbona haujanijibu? Upo tayari? DORCAS: Tayari nini? MIMI: Kuwa na mimi. DORCAS: Mmmh! Unataka nipigwe tu. MIMI: Na nani tena? DORCAS: Msichana wako. MIMI: Yupi? DORCAS: Una marafiki wengi sana Nyemo, kuna wasichana wengine wanapenda sana kufuatilia hadithi zako, sasa unafikiri watajisikiaje kama wakiona nipo na wewe? MIMI: Watajisikia kawaida kwani hawajawahi kuniambia kwamba wananipenda. DORCAS: Hahaha! Hapana bwana Nyemo. Kwa hiyo wangekwambia? MIMI: Ningekataa. DORCAS: Kwa nini sasa? MIMI: Kwa sababu moyo wangu upo kwako. DORCAS: Nyemo unataka kunitafutia ugomvi bwana. Sipendi maneno maneno bwana. Nianze kuzungumziwa sana kisa natoka na wewe. Wasichana sisi tuna mambo sana Nyemo. Acha niwe peke yangu kwa sasa. MIMI: Hicho ni kitu ambacho sitaki kitokee. Najua kwamba inawezekana kuna msichana au wasichana wanapenda kuwa na mimi, okey, hiyo ni hali ya kawaida kutokea facebook japokuwa sitaki itokee kwa sababu napenda kufanya mambo yangu kwa uhuru facebook, lakini watakwambia maneno gani na wakati uhusiano wangu ni kati yangu na wewe tu. Usiwaogope bwana, wataongea sana mchana, usiku watalala tu. DORCAS: Ila kila siku nitakuwa nikiumia sana Nyemo. MIMI: Kivipi? DORCAS; Mtu akitokea na kuanza kukuita ‘wangu, kipenzi, sweetie’ na majina mengine kwenye comment, unafikiri nitafurahia? MIMI: Ni majina ya kawaida tu, labda uwe na wivu kupitiliza. DORCAS; Wivu ndio mapenzi Nyemo. Kama nisipojisikia wivu kwako, hiyo inamaanisha sina mapenzi kwako. Ili nijulikane kama nina mapenzi, wivu muhimu. MIMI: Kumbe ndivyo ilivyo? DORCAS: Yeah! MIMI: Sawa, nimekuelewa. Nipe jibu la uhakika sasa….upo tayari? DORCAS: Dah! MIMI: Nini tena? DORCAS: Mambo magumu sana Nyemo. Nauonea huruma moyo wangu tu. MIMI: Usijali. Nitaujali na kuulinda. DORCAS: Kabla sijakujibu naomba nikuulize swali moja. MIMI: Uliza tu. DORCAS: Umekwishawatongoza wasichana wangapi humu facebook? MIMI: Mmoja tu. Wewe. DORCAS: Hahaha! Na umekwishawahi kutongozwa na wasichana wangapi humu facebook? MIMI: Hakuna hata mmoja. DORCAS: Una rekodi ya kutongozwa na msichana yeyote maishani mwako? MIMI: Hapana. DORCAS: kwa hiyo huwa unatongoza wewe tu? MIMI: Maswali yamekuwa mengi kweli Dory. DORCAS: Hahaha! Mbona unaonekana kulikimbia swali. Nijibu kwanza. MIMI: Kwa hiyo kisa nataka cha uvunguni, kwanza sharti niiname? DORCAS: Ndio. MIMI: Sijazoea kutongoza. Huwa najisikia aibu sana. DORCAS: Sasa mbona mimi umenitongoza. MIMI: Sijakutongoza. DORCAS: kumbe umefanya nini hapo? MIMI: Nimekukumbusha tu juu ya upendo ambao nilikuwa nao juu yako toka zamani. DORCAS: Hahaha! Wewe mwanaume mjanja sana. Yaani unakwepa kwepa. MIMI: Huo ndio ukweli. Upo tayari? DORCAS: Naomba unipe muda. MIMI: Muda! Wa nini tena? DORCAS: Kujifikiria. MIMI: Yaani hata ukumbusho wangu pia unahitaji kufikiriwa? DORCAS: Ndio. MIMI: Ukinijibu hapa hapa kuna nini? DORCAS: Kuna mengine si ya kujibu haraka haraka Nyemo. MIMI: Kwa hiyo unakwenda kuomba ushauri kwa mama? DORCAS: Umejuaje! Si unajua kila kitu lazima nimshirikishe. MIMI: Hebu acha zako. Niambie basi kwanza nijue ni nini hatma yangu, kama kujiua au kuendelea kuvuta pumzi. DORCAS: Hahaha! Ujiue kisa mapenzi? MIMI: Yeah! Sasa kama mtu unampenda halafu yeye hakupendi, unategemea nini? Kujiua tu. DORCAS: Sasa mbona hukujiua toka zamani? MIMI: Nilikuwa sina akili ya kujiua. Ila sasa hivi ninayo. Ukinikataa tu, najiua, nishachoka maisha ya kukataliwa na mtu mmoja. DORCAS: Owkey..Usijali. Tutaongea zaidi baadae. Nataka kwenda kusuka. MIMI: Daah! Naomba kwanza unipe jibu langu. DORCAS: Itakuwa ngumu kwa sasa. Unaonaje tukionana baadaye. MIMI: Tuonane wapi? DORCAS: Unapajua nyumbani? MIMI: Hapana. DORCAS: Njoo hapa magomeni Mapipa then nitakufuata kituoni. MIMI: Sasa hivi? DORCAS: Usiwe na haraka. Nikimaliza kusuka nitakushtua. MIMI: Poa. DORCAS: Kwa heri. MIMI: Ila namba yangu si unayo? DORCAS: Sina. Hebu nipatie. MIMI: 0716 008866 DORCAS: Mtoto wa Tigo. MIMI: Kama kawa mchumba. DORCAS: Basi baadae. MIMI: Pwaxxxxx   Kilichofuata baada ya hapo ni Dorcas kutoka online. Moyoni nilijisikia amani kupita kawaida, furaha ambayo ilikuwa imetoweka ikaanza kurudi. Dorcas yule ambaye nilikuwa nikimfuatilia kwa kipindi kirefu, leo hii alikuwa ameamua kukutana nami na kisha kukaa pamoja na kuzungumza. Kiukweli nilikuwa katika mudi nzuri sana, yaani kwa hali ya furaha ambayo nilikuwa nayo katika kipindi hicho, hata kama ungekuja kwangu na kuniambia nikukopeshe 10,000/=, nisingekukopesha, ningekupa kama rafiki yangu kutokana na furaha ambayo nilikuwa nayo.   Hii facebook hii…yaani hawa wasichana hawawezi hata kujishika kabisa. Kipindi cha nyuma kabla ya kuanza kumfuatilia Dorcas, wala hawakuwa wakinifuata fuata ila baada ya hapo ndipo nao wakaonekana kubadilika kiasi ambacho mpaka nikaanza kuiona facebook kuwa chungu. Mapenzi haya + facebook = bado nusu yanitoe roho hasa mara baada ya kuingia katika mahusiano na huyu Dorcas ambaye kwa wakati huo nilikuwa namuita moyoni ‘QUEEN OF MY HEART’.   Nilionekana kuwa mwingi wa presha, muda wote nilikuwa naiangalia simu yangu tu, sikujua ni muda gani ambao mtoto Dorcas angepiga simu ile. Macho yangu yalikuwa kodokodo kila wakati. Nilikuwa na hamu kubwa ya kuonana na Dorcas kuliko mtu yeyote katika dunia hii.   Kuna kitu kimoja ambacho kilikuwa kikiniudhi sana na ninaamini kwamba hata wewe kimekwishawahi kukutokea mara nyingi sana. Utakuta mtu unasubiri simu ya mtu muhimu sana, halafu katika kipindi hicho hicho mtu mwingine anaanza kukupigia simu, unakuwa kwenye hali gani? Sasa hicho ndicho kilichokuwa kikinitokea katika wakati huo.   Sijakaa vizuri, Vonso, rafiki yangu kapiga, sijakaa vizuri, Shedrack Joshua kapiga, sijakaa vizuri, utakuta nae Muksin Muhinga nae kapiga, siku hiyo nilikuwa nikikasirika sana kiasi ambacho nilitamani kuwatukana. Katika kipindi hicho, sikutaka kupokea simu ya mtu yeyote yule, simu ambayo nilikuwa nikitaka kuipokea ni ya msichana Dorcas tu. Saa 11:20 jioni, simu yangu ikaanza kuita tena, nilipoiangali, ilikuwa ngeni, unafikiri nilifikiri nani hapo? Nilipoipokea, sikio langu likakutana na sauti nzuri, sauti nyororo ambayo sidhani kama nilikwishawahi kuisikia sehemu yoyote zaidi ya waimba kwaya hasa wale wanaoimba sauti ya kwanza. Alikuwa Dorcas.   DORCAS: Mambo! MIMI (Huku nikitoa tabasamu kana kwamba Dorcas alikuwa akiniona): Poa. U mzima? DORCAS: Mzima. Otea unaongea na nani. MIMI: Naongea na Malaika wangu, Dorcas. DORCAS: Hahaha! Upo wapi? MIMI: Nipo home. DORCAS: Unaweza kuja sasa hivi au upo bize? MIMI: Naweza. Sipo bize wala nini, yaani hapa nilikuwa nasubiria simu yako tu. DORCAS: basi poa. Nakusubiria hapa Mapipa. MIMI: Poa. (Nikakata simu)   Vitu vingine si lazima nikuambie ni kwa jinsi gani katika kipindi hicho nilikuwa na uharaka. Nilivaa nguo fasta fasta halafu mbaya zaidi, kila nguo niliyokuwa nikiivaa niliiona kuwa haijanikaa vizuri na wakati siku nyingine zilionekana kunikaa vizuri. Kiu yangu katika kipindi hicho ilikuwa ni kumuona Dorcas kwa mara nyingine tena, katika kipindi ambacho ningekaa nae chini na kuanza kuzungumza nae.   Nilipotoka nyumbani, sikuaga, nikachoma mazima na kukimbilia tigo pesa. Sikutaka kwenda mifuko mitupu au labda ningekuwa nakutana na rafiki yangu Babi De Councious. Nikatoa shilingi elfu kumi na tano na kisha kuchukua bajaji.   Nadhani hiyo ndio ilikuwa siku ya kwanza kukodi bajaji kutoka Tandale mpaka Magomeni. Japokuwa Dorcas alikuwa akiijua hali yangu ni ya kawaida lakini siku hiyo nilitaka kuonekana tofauti kidogo. Bajaji ilichukua dakika tano, ikafika Magomeni Mapipa na kisha kuteremka.   Macho yangu yalipotua kwa Dorcas, alionekana kuwa mrembo sana asikwambie mtu. Alikuwa amevaa kipedo cha jinzi fulani zile laini laini, kishati kidogo cha rangi ya pinki pamoja na raba fulani simpo sana huku kichwani akiwa amevaa kofia fulani za kisista duu.   MIMI: Duh! DEREVA BAJAJI: Vipi? MIMI: Demu mwenyewe yule pale. Kulalaleki, kawa mkali ile mbaya. DEREVA BAJAJI: Yupo wapi? Yule mwenye hijabu? MIMI: Hapana. Yule aliyevaa kipedo. DEREVA: Duuuh! MIMI: Vipi? DEREVA BAJAJI: Mmmh! Yule demu mkali aisee. MIMI: Ndio huyo bwana. Chukua kwanza hii hela yako then tutaonana nyumbani (Nilimwambia huku nikimgawia fedha zake) DEREVA BAJAJI: Poa (Akaipokea fedha ile na kisha mimi kushuka chini)   Nikaanza kupiga hatua kumfuata Dorcas, kwa mbali nilikuwa nikitetemeka huku kijasho chembamba kikinitoka. Kwa mbwembwe zake, Dorcas aliponiona, akapiga uyowe mkubwa na kisha kuja kunikumbatia kwa furaha. Nilijisikiaje aibu. Dorcas alikuwa akinukia kupita kawaida, pafyumu yake ambayo alikuwa amejipulizia siku hiyo nadhani sijawahi kuisikia sehemu yoyote ile.   MIMI: Mmmh! Unanukia vizuri (Nilimwambia karibu na sikio lake huku akiwa kanikumbatia) DORCAS: Asante MIMI: Natamani nikubebe juu, na hivi ulivyokuwa mwembamba. DORCAS: Hahaha (Alitoa kicheko fulani cha kizushi na kisha kujitoa kifuani mwangu)   Kilichofuata mahali hapo ni kwenda kwenye ule mghahawa uliokuwa katika jengo lililokuwa na internet ya Virus na KISHA Dorcas kumuita mhudumu.   DORCAS: naomba Mirinda nyeusi pamoja na kababu. Msikilize na huyo mume wangu (Dorcas alimwambia mhudumu yule) MIMI: Naomba bia. Pombe kali yenye kilevi kuanzia 5%. DORCAS: Wewe Nyemo. MIMI: Naam. DORCAS: Wewe si umeokoka. MIMI: Najua. DORCAS: Pombe ya nini sasa? MIMI: Hahaha! Nilikuwa namzingua. Naomba uniletee juisi ya maembe pamoja na chipsi. MHUDUMU: Aweke kila kitu kwenye chipsi? MIMI: Yeah! Mwambie aweke kila kitu. Mpaka sumu. MHUDUMU na DORCAS: Hahahaha (Mhudumu akaondoka mahali hapo)   Hiyo ndio tabia yangu, huo ndio muonekano wangu wa kila siku. Mara kwa mara ninaonekana kuwa mcheshi huku nikijaa utani bila kutambua kama hiyo ni siku ya kwanza kukutana nawe au la. Kila nilichokuwa nikikifanya mahali hapo ni kumruhusu Dorcas aendelee kujua kwamba sikuwa nimebadilika, nilikuwa Nyemo yule yule ambaye nilikuwa nikimfuatilia toka kitambo. Vinywaji na vyakula vikaletwa mahali pale na kisha kuanza kula.   DORCAS: Naomba uniambie kuhusu mapenzi (Dorcas aliniambia huku akiniangalia) MIMI: Mapenzi ni kama kiti cha basi. DORCAS: Sipendi kusikia msemo huo. MIMI: Okey! Mapenzi ni kama maua. DORCAS: Bado sijaridhika. MIMI: Sasa unataka nikwambie mapenzi ni kama nini? DORCAS: Jaribu kutunga. Wewe si mtungaji. MIMI: Okey! Mapenzi ni kama darasa. DORCAS: Ndio kwanza nasikia kwako. MIMI: Si umeniambia nitunge? DORCAS: Yeah! Endelea. MIMI: Tufanye mapenzi ni darasa, wewe ni mwanafunzi. Mara kwa mara unapokwenda shule, unapenda kuliweka darasa katika hali ya usafi. Unapofunga shule au kumaliza, huwa unatamani sana kama ungerudi shuleni, si ndio hivyo? DORCAS: Ndio. MIMI: Sawa na mapenzi. Unapokuwa haupo kwenye mapenzi, huwa unatamani sana urudi tena katika mapenzi kama unavyotamani kurudi darasani unapomaliza shule. DORCAS: Kidogo naanza kukupata. MIMI: Unapopata nafasi ya kurudi darasani, unajisikia mwingi wa furaha kwa sababu unakutana na watu tofauti tofauti ambao ulikuwa umezoeana nao. Si ndio hivyo? DORCAS: Yeah! MIMI: Unapokuwa darasani unaongea na wenzako kwa furaha, mwalimu wa somo usilolipenda anapoingia, huwa unajisikiaje?   ITAENDELEA..

No comments